Singida Black Stars FC yaanika malengo yake

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:20 PM Apr 04 2024
Picha ya kuunganishwa kushoto wachezaji wa Ihefu, ambayo kwa sasa itajulikana kama Singida Black Stars.
MAKTABA
Picha ya kuunganishwa kushoto wachezaji wa Ihefu, ambayo kwa sasa itajulikana kama Singida Black Stars.

BAADA kubadilishwa jina kutoka Ihefu FC na kuitwa Singida Black Stars, uongozi wa timu hiyo umesema sababu ya kufikia uamuzi huo imetokana na kuitaka klabu hiyo kuwa karibu na mashabiki wao wa mkoa wa Singida.

Mabosi wa timu hiyo pia wameweka wazi tayari wamekamilisha taratibu zote za usajili katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

Mkurugenzi wa Utawala wa Singida Black Stars, Muhibu Kanu, alisema nia na malengo ya kubadilisha jina ni kuunganisha timu kwa wananchi wote wa Singida baada ya kuhamia mkoani humo tangu Februari, mwaka huu.

"Nia na malengo ya kubadilisha jina ni kuiunganisha timu na wananchi wote wa Mkoa wa Singida, hasa ikizingatiwa kwa sasa imehamisha maskani yake kutoka ilipokuwa na kuja mkoani hapa.

Taratibu zote za usajili wa jina hilo zimeshamalika kwa kufuata mwongozo, kanuni na taratibu zote nchini, TFF na BMT na timu yetu hii tumelenga katika kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana wa nchi yetu ili kuinua maisha yao na kutimiza ndoto zao kupitia vipaji walivyonavyo," alisema Kanu.

Alisema ana imani kubwa wataendelea kushirikiana na wadau wote na kila mmoja kwa nafasi yake ili kuendeleza mpira wa miguu wa Tanzania.

Ihefu ilihamia mkoani humo, na kuamua kucheza mechi zake za Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa CCM Liti, Singida.

Na hii ilitokea baada ya baadhi ya wachezaji wa Singida Fountain Gate kuhamishwa katika klabu ya Ihefu kipindi cha usajili wa dirisha dogo.

Kwa sasa kikosi cha Singida Black Stars kiko Mwanza tayari kwa mechi ya Kombe la FA dhidi ya Tabora United itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.