MAUAJI KADA CCM: Mahakama Kuu yawaachia huru wanachama watatu wa CHADEMA

By Elizabeth John , Nipashe
Published at 10:09 AM Jan 01 2025
Nje ya mahakama.

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Iringa imewaachia huru wanachama watatu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya mauaji ya kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Emmanuel Mlelwa.

Hao ni Geogre Sanga, Goodluck Mfuse na Optatus Nkwera walioshtakiwa kwa mauaji ya Emmanuel Mlelwa yaliyofanywa Septemba 2020.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 5236/2024, upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali Cesilia Mkonongo, akisaidiwa na Geres Tesha na Elise James huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na Wakili Dickson Matata, akisaidiwa na Franki Ngafumika, Innocent Kibadu na Neema Msafiri.

Akisoma hukumu hiyo jana kwa njia ya mtandao, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa inayojumuisha pia mkoa wa Njombe, Danstan Ndunguru, alisema kuachiwa huru kwa watuhumiwa hao kunatokana na upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha kosa dhidi ya Geogre Sanga na wenzake.

Alisema upande wa utetezi ulikuwa na mashahidi watano huku upande wa Jamhuri ukiwa na mashahidi 14 na kwamba hakuna shahidi aliyeona watuhumiwa wakitenda kosa la mauaji ya Emmanuel Mlelwa.

Jaji huyo alisema kuwa katika ushahidi wa kimazingira uliowasilishwa mahakamani na upande wa Jamhuri, haukuwa na muunganiko mzuri usioacha shaka.

Alisema ushahidi huo wa kimazingira umeacha shaka iliyofanya mahakama ishindwe kubaini iwapo ushahidi wa kimazingira uliotolewa, kuwaunganisha watuhumiwa na kosa ni sahihi au la.

Jaji Ndunguru alisema ushahidi wa kisayansi wa uchunguzi wa vinasaba ulioletwa mahakamani umeshindwa kutumika kuwatia hatiani washtakiwa hao kwa kuwa sampuli za vinasaba zilizopelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, wakati zinachukuliwa kulikuwa na ukiukwaji taratibu za kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Vinasaba ya Mwaka 2009.

Baada ya hukumu hiyo, Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa ya CHADEMA, Joseph Mbilinyi, maarufu Sugu, alitaka serikali kumaliza kesi alizoziita "za wafungwa wa kisiasa" katika maeneo mengine nchini, ikiwamo ya Kibaha mkoani Pwani, akidai zinachafua taswira ya nchi.