Simba yatua kwa kipa Matampi wa Coastal

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:08 AM May 14 2024
news
Picha: Maktaba
Golikipa Ley Matampi.

BAADA ya taarifa za kumpa mkataba wa awali beki wa kati ya Coastal Union, Lameck Lawi, klabu ya Simba imeendelea kuiganda timu hiyo na sasa wanafanya mpango wa kumsajili golikipa Ley Matampi raia wa Jamhuri ya Kidemkokrasi ya Congo, ambapo kama mambo yatakwenda vyema anaweza kuvaa uzi mwekundu msimu ujao.

Habari kutoka ndani ya zinasema Matampi, ameonekana kulivutia benchi la ufundi la timu hiyo pamoja na mabosi wake, hivyo kumuweka kwenye orodha ya wachezaji wanaowahitaji kama itashindikana kumbakisha golikipa wao Ayoub Lakred raia wa Morocco.

Awali klabu hiyo ilikuwa na mpango wa kumsajili kipa Mcameroon, Joseph Fabrice Ondoa ambaye anacheza soka lake nchini Ufaransa katika klabu ya Nimes Olympique inayoshiriki ligi ya National, ambayo ni Ligi Daraja la Pili nchini humo.

"Hakuna uhakika wa moja kwa moja kama Lakred anaweza kubaki au la. Hata kama anataka kubaki, lakini klabu nayo inaweza kuweka masharti ambayo tunaweza kushindwana, kwa hiyo kama ikitokea hatukuelewana, basi mbadala atakuwa ni Matampi, benchi la ufundi na uongozi umeridhishwa na kiwango chake," kilisema chanzo chetu ndani ya klabu hiyo.

Chanzo hicho kinasema tayari mazungumzo yameanza na yeye mwenyewe ameonekana kuvutiwa na ofa, huku klabu ya Simba ikiamini hakutokuwa na kipingamizi chochote kutoka kwenye klabu yake ya Coastal.

Kipa huyo ambaye aliwahi kuidakia timu ya taifa ya DR Congo, anashika nafasi ya pili nyuma ya kipa wa Yanga, Djigui Diarra, kukaa langoni mechi nyingi bila kuruhusu bao, 'clean sheets,' akiwa nazo 12, nyuma ya raia huyo wa Mali ambaye ana 'Clean sheet' 13.

Coastal, ilimsajili kipa huyo kutoka klabu ya Renaissance ya DR Congo, ambapo mbali na klabu hiyo, amezichezea klabu zote kubwa nchini humo, AS Vita, TP Mazembe, na DC Motema Pembe , pia aliwahi kucheza soka la kulipwa nchini Lebanon kwenye klabu ya Al-Ansar.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema ingawa wanatarajia kufanya usajili mkubwa mara tu Ligi Kuu msimu huu itakapomalizika, lakini kwa sasa siyo wakati wa kuzungumzia chochote kuhusu hilo.

"Kwa sasa bado tupo kwenye ligi, hatuzuii tetesi za usajili, lakini ukweli wa kila kitu utabainika pale ligi itakapomalizika, nani atatoka na nani ataingia Simba, ila ukweli kwamba tunataka kufanya usajili mkubwa," alitamba Ahmed.