Simba, Yanga, Azam kitaeleweka dimbani leo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:44 AM Feb 07 2026
news
Picha Mtandao
Simba, Yanga, Azam kitaeleweka dimbani leo

WAWAKILISHI wa Tanzania katika mashindano ya kimataifa ya CAF, Simba, Yanga na Azam FC leo watashuka katika viwanja tofauti kusaka pointi tatu muhimu zitakazowavusha kwenda hatua ya robo fainali.

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga watakuwa ugenini Morocco kuwakabili AS FAR Rabat katika mechi ya Kundi B ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa kuanzia saa 4:00 usiku.

Yanga yenye pointi tano sawa na wapinzani wao wanahitaji ushindi ili kuweka mguu mmoja ndani katika hatua inayofuata ya michuano hiyo, ikishuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 waliopata kwenye mchezo wa raundi ya kwanza.

“Tumebeba kila aina ya silaha inayotakiwa kuhakikisha tunapata ushindi au pointi moja katika mechi hii, hii itatupa wepesi kuelekea mechi ya mwisho,” Ali Kamwe, Msemaji wa Yanga ameiambia Nipashe Digital.

Simba ambao msimu huu imekuwa na matokeo mabaya katika hatua ya makundi itashuka dimbani ugenini kuwakabili Atletico Petroleos kuanzia saa 1:00 usiku.

Mnyama anahitaji kumaliza mechi zake kwa heshima kufuatia matokeo mabaya aliyopata kwenye michezo iliyotangulia.

Wakati huo huo Azam FC wao watawakaribisha AS Maniema kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) katika mechi ya Kundi C ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mechi hiyo itachezwa kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.