Simba yaahidi raha, Yanga hapa kazi tu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:17 PM Feb 11 2026
Kikosi cha Simba kikiwa mazoezini.
Picha: Simba
Kikosi cha Simba kikiwa mazoezini.

BAADA ya kushindwa kusonga mbele katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba imesema imejiandaa kuonesha ‘ukubwa’ na soka la burudani itakapowavaa KMC katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, amesema hawahitaji kupata ushindi pekee, bali wamejiandaa kucheza vizuri na kutawala mechi hiyo.

 Barker alisema awali katika kikosi chake kulikuwa na tatizo la wachezaji kucheza taratibu wanapokuwa kwenye michezo ya Ligi Kuu na wanaongeza kasi wanapokwenda kucheza michezo ya kimataifa, lakini mtazamo huo ameutoa na kuufuta.

"Tumerejea kucheza ligi baada ya kushindwa kufuzu hatua ya robo fainali, hii itakuwa mechi ambayo tunatakiwa kuwarudishia imani mashabiki wetu, tunatakiwa kuonesha sisi ni timu kubwa, hatudharau timu hii, lakini tunakwenda tukiwa imara.

 Tunahitaji kucheza mechi hii vizuri, kucheza soka safi, kutawala mchezo na kupata ushindi kama ambavyo malengo yetu yalivyo," alisema Barker.

 Aliongeza alichokifanyia kazi ni utumiaji wa nafasi ambapo kikosi hicho hupoteza nafasi nyingi.

"Nimewaambia wachezaji wangu wawe wanajiamini wanapokuwa ndani ya eneo la hatari ili kufunga kwa ufasaha, nilichofurahi kwa sasa nina wachezaji wapya ambao wamenionyesha ni wabunifu, watengenezaji wazuri wa nafasi rahisi, hivyo inaweza kusaidia," aliongeza kocha huyo.

Wakati huohuo, Yanga imeziomba klabu zote zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara na zile za Ligi ya Championship kuiombea timu yao ili ifuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema kwa hali iliyopo sasa hakuna timu nyingine nchini ambayo yenye angalau uhakika wa kusonga mbele hatua ya makundi isipokuwa Yanga tu.

 "Tunaomba watuombee ili Yanga iheshimishe Tanzania, angalu kama nchi tuwe na timu moja katika hatua ya robo fainali michuano ya kimataifa," Kamwe alisema.

 Aliongeza timu yao haitakuwa na mapumziko na badala yake inaendelea na maandalizi kwa ajili ya mechi yao ya mwisho dhidi ya JS Kabylie kutoka Algeria itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

 "Buba ameshafika, ataungana na wenzake kwenye maandalizi, siku ya kuondoka kwenda Zanzibar hatuweki wazi, huu ni mkakati wetu, hii mechi ni muhimu lazima tuwe na tahadhari," alisema  Kamwe.