Simba, Azam vitani ugenini

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 07:29 AM Sep 26 2024
Simba, Azam vitani ugenini
Picha:Mtandao
Simba, Azam vitani ugenini

BAADA ya kufuzu hatua ya makundi ya mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika kibabe, Simba inatarajia kushuka ugenini kuwakabili Azam FC katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Ligi Kuu ya Tanzania Bara imehamia kwa muda Visiwani Zanzibar baada ya wenyeji wa mchezo huo, Azam FC kuchagua kuutumia uwanja huo uliofanyiwa ukarabati hivi karibuni.

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, aliliambia gazeti hili hawatarajii mchezo huo kuwa mwepesi kutokana na ubora wa kikosi cha wapinzani wao Azam FC.

"Azam ni timu nzuri, wanawachezaji wenye uwezo mkubwa, nadhani utakuwa mchezo mzuri na wenye upinzani," alisema Fadlu.

Kocha huyo alisema amekiandaa vizuri kikosi chake kuelekea katika mchezo huo utakaochezwa kuanzia saa 2:30 usiku.

"Tumetoka kwenye mchezo mgumu dhidi ya Al Ahly Tripoli, lakini tumefanya maandalizi kwa ajili ya mchezo huu, ni muhimu sana kwetu kupata ushindi ili tuendelee pale tulipoishia katika michezo yetu ya Ligi Kuu," Fadlu alisema.

Naye Kocha Mkuu wa Azam FC, Rashid Taoussi, ambaye atakuwa anakutana na Simba kwa mara ya kwanza tangu ajiunge na timu hiyo alisema amejindaa vizuri kuwakabili Wekundu wa Msimbazi ingawa amekiri anatarajia mchezo utakuwa mgumu.

Taoussi alisema ugumu wa mechi hiyo unatokana na aina ya mpinzani wanayetarajia kukutana naye.

"Yote kwa yote tumejiandaa vizuri, tunataka pointi tatu ingawa  mchezo hautakuwa mwepesi, wachezaji wangu wapo tayari kwa ajili ya mchezo huu muhimu," alisema Taoussi.

Kocha huyo ameanza kuifundisha Azam FC hivi karibuni akirithi mikoba iliyoachwa na Yousouph Dabo, ambaye aliondolewa  kutokana na matokeo yasiyoridhisha.

Azam yenye maskani yake Chamazi, imecheza mechi nne na imejikusanyia pointi nane wakati Simba yenye pointi sita imeshuka dimbani mara mbili tu wakati Singida Black Stars inaongoza katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 12 baada ya kushinda michezo yake yote minne iliyocheza.