WAKATI Rais Samia Suluhu Hassan leo anatimiza siku 100 tangu alipoapishwa tena kuiongoza Tanzania, kumekuwa na matukio mbalimbali chanya yakukumbukwa, rekodi za kuvutia, maendeleo, maono na neema kwa wanamichezo mbalimbali hapa nchini. Mafanikio hayo ya wanamichezo yameenda sambamba na ahadi alizozitoa Rais Samia za kuhakikisha Tanzania inafanya vizuri katika mashindano yote wanayoshiriki.
Ilikuwa ni Desemba 30, mwaka jana, Timu ya Taifa (Taifa Stars), ilipotinga hatua ya 16 bora kwa mara ya kwanza tangu Tanzania kupata Uhuru mwaka 1961, katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), yaliyomalizika hivi karibuni huko Morocco.
Kiwango kizuri kilichooneshwa na Stars katika fainali hizo kilitokana na kiongozi huyo namba moja kushiriki kikamilifu kwenye hamasa na maandalizi ya kikosi hicho kilichokuwa chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi.
Taifa Stars imeshiriki fainali za AFCON mara tatu ikianza mwaka 1980, 2019 na 2023, lakini timu hiyo haikufanikiwa kuvuka hatua ya makundi, lakini ilifanya hivyo wakati huu, pale ilipotoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Tunisia na kusonga mbele kwenye michuano hiyo, ndani ya siku 100 za Rais Samia.
Kwa heshima ambayo nyota wa Stars waliipa Tanzania, rais huyo aliwaalika wanamichezo mbalimbali Ikulu, Dar es Salaam kuwapongeza kwa kufanya vyema na kuliletea sifa taifa, lakini gumzo lilikuwa ni ilivyowashangaza wadau wengi wa soka kwa kuonesha kiwango bora zaidi ya ilivyotarajiwa.
“Tunajua kila kitu kilichotokea, dunia imeona, mmeiheshimisha Tanzania,” Rais Samia aliwaambia wachezaji wa Stars katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na wanamichezo mbalimbali.
Huku Alphonce Simbu, akiwa na ‘joto’ la kutwaa medali ya dhahabu katika mashindano ya dunia ya riadha yaliyofanyika Septemba, mwaka jana katika jiji la Tokyo, Japan akiwa ni Mtanzania kwa kwanza kutwaa medali kwenye michuano hiyo, wiki iliyopita mwanariadha huyo ameshinda medali ya fedha katika mbio za kilomita 21 za Burj2Burj zilizofanyika Dubai, Falme za Kiarabu Jumapili iliyopita.
Nuru ya Rais Samia iliendelea kufanya kazi kupitia hamasa ya 'goli la mama', wakati klabu za hapa nchini zilipokuwa zikicheza mechi za mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho kwa kununua bao kwa gharama ya kuanzia Sh. Milioni tano, kila wanapoibuka na ushindi kwenye mechi husika.
Lengo lilikuwa ni kuendelea kuzihamasisha timu hizo kufanya vizuri na matokeo yake Tanzania kwa mara ya kwanza ilifanikiwa kuwa na wawakilishi wanne kwenye hatua ya makundi.
Wawakilishi hao si wengine ni Simba, Yanga, Azam zote za Dar es Salaam na Singida Black Stars kutoka mkoani, Singida.
Miaka mingine wawakilishi hao wa Tanzania walionekana wasindikizaji katika mashindano hayo ya CAF huku wadau wa soka wakishuhudia timu za Kaskazini zikitawala.
Ndani ya siku hizo pia, Timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars), imefuzu kwa mara ya tatu kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (WAFCON 2026), ambazo pia zitafanyika Morocco baadaye mwaka huu.
Timu ya Taifa ya Wasichana ya umri chini ya miaka 15 imetwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati huku mabingwa watetezi kwa upande wa wavulana wakimaliza kwenye nafasi ya pili katika michuano ya CECAFA U-15.
Akidhihirisha yeye ni shabiki namba moja wa Taifa Stars, Rais Samia, amehakikisha kasi ya ujenzi wa Uwanja wa Arusha ulioko katika eneo la Olmot, utakatumika kwenye AFCON 2027 unakamilika kwa wakati, kasi ikiongezeka na sasa imefikia zaidi ya asilimia 80 kwa serikali yake kuwekeza kiasi cha Sh. bilioni 286.
Kama vile haitoshi, imeshuhudiwa pia ujenzi wa Uwanja wa Fumba ulioko Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar ukienda kwa kasi kubwa na ameahidi utakamilika ifikapo Julai, mwaka huu tayari kwa matumizi yaliyokusudiwa.
Uwanja huo utakuwa na uwezo wa kuingiza watu 36,000 kwa wakati mmoja na uwezo wa kuegesha magari zaidi ya 2,000.
Mabondia pia hawajaachwa, wamekuwa wakipata zawadi mbalimbali za fedha waliposhiriki mapambano ya ‘KO ya Mama’ yakiwa na lengo la kuwaandaa kwa ajili ya kushiriki mapambano mengine ya kimataifa.
Ilikuwa ni Desemba 26, mwaka jana, Hassan Mwakinyo, kutoka jijini, Tanga alitwaa mkanda unaotambuliwa Shirikisho la Ngumi Afrika na WBO kwa kumchapa bondia kutoka Nigeria.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED