Serikali yabariki marekebisho Katiba ya Simba

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 02:17 PM Feb 18 2026
Mashabiki wa Simba
Picha: Mtandao
Mashabiki wa Simba

Serikali imeidhinisha rasmi marekebisho ya Katiba ya Klabu ya Simba, baada ya kukamilika kwa mchakato wa kisheria uliokuwa chini ya Msajili wa Vyama vya Michezo Tanzania.

Hatua hiyo sasa inatoa nafasi kwa klabu hiyo kuendelea na mabadiliko ya uendeshaji na kukamilisha mchakato wake.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 18 jijini Dar es Salaam,  Msajili wa Vyama vya Michezo nchini, Abel Ngilangwa, amesema marekebisho hayo yamefanyika kwa kuzingatia sheria na kanuni zote zinazosimamia vyama vya michezo nchini.

“Napenda kuufahamisha umma kuwa mchakato wa uchambuzi, tathimini na uidhinishaji wa marekebisho ya Katiba ya Klabu ya Simba umekamilika kwa mujibu wa Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa Sura ya 49 na Kanuni zake,” amesema Ngilangwa. 

Amesema serikali imejiridhisha kuwa marekebisho hayo hayatathiri usalama, hayachochei migogoro miongoni mwa wanachama na hayapingani na sheria za nchi, hivyo yameidhinishwa rasmi. 

Amesema miongoni mwa maboresho yaliyoidhinishwa ni kuweka wazi nafasi ya Simba Sports Club Company Limited kama chombo kitakachosimamia masuala ya kibiashara na kiutendaji, huku umiliki wa hisa ukiendelea kuwa chini ya Baraza la Wadhamini kwa niaba ya wanachama.

Februari 16 mwaka huu, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, alimwagiza Msajili wa Vyama vya Michezo kuhakikisha mchakato wa Katiba ya Simba unakamilika kabla ya mwezi huu kuisha.