Shirikisho la muungano wa vyama vya soka Ulaya, UEFA, na Real Madrid viko tayari kumaliza mzozo wao wa kisheria kuhusu Ligi Kuu mpya ya Klabu za Ulaya (Super League), kwa mujibu wa ESPN.
Real Madrid walibaki kama klabu pekee iliyosajiliwa kwenye mashindano hapo yaliyopendekezwa kujitenga na yale ya UEFA, baada ya miamba wenzao wa Hispania, Barcelona kujiondoa kwenye mradi huo wiki iliyopita.
Real ilikuwa imeomba "fidia kubwa" kutoka kwa UEFA baada ya baraza hilo linaloongoza soka barani Ulaya kushindwa kwenye rufaa ya mahakama kuhusu mradi wa Super League mnamo Oktoba 2025.
Hata hivyo, UEFA, Umoja wa Klabu za soka Ulaya (EFC) na Real Madrid walisema Jumatano kwamba "makubaliano ya kanuni" yamefikiwa "kwa manufaa ya soka la klabu za Ulaya".
Klabu 12 za Ulaya awali ziliunga mkono mashindano hayo ili kujitenga na UEFA mwaka 2021, kabla ya mradi huo kushindikana.
Taarifa ya pamoja ya UEFA, EFC na Real Madrid ilisema: "Baada ya miezi kadhaa ya majadiliano yaliyofanywa kwa maslahi ya soka la Ulaya, UEFA, EFC, na Real Madrid tunatangaza kwamba, tumefikia makubaliano ya kanuni kwa ajili ya ustawi wa soka la klabu za Ulaya.”
Klabu za Ligi Kuu England, Arsenal, Chelsea, Liverpool, Manchester City, Manchester United na Tottenham Hotspur zilijisajili katika mradi huo, lakini zote zilijiondoa ndani ya saa 72 baada ya upinzani mkubwa kutoka kwa mashabiki wao.
Barcelona na Real Madrid zilibaki katika mradi huo hadi Oktoba 2025, wakati rais wa Barcelona, Joan Laporta aliposema klabu hiyo inajitoa na wiki iliyopita ilitangaza rasmi kujiondoa.
CHANZO: ESPN
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED