Ramovic: Wachezaji wangu hawako fiti

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:31 AM Nov 28 2024
Ramovic: Wachezaji wangu hawako fiti
Picha: Yanga
Ramovic: Wachezaji wangu hawako fiti

BAADA ya kukaribishwa na kichapo, Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, amesema timu yake ilipoteza mechi ya kwanza ya hatua ya makundi ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal kutoka Sudan kwa sababu wachezaji wake walikosa utimamu wa mwili na pumzi ya kutosha kumudu kucheza dakika zote 90.

Yanga ilipoteza mechi hiyo kwa kufungwa mabao 2-0, mchezo wa Kundi A uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam juzi.

Ramovic, alisema tatizo aliloliona katika kikosi chake ni wachezaji kutomudu kucheza kwa nguvu inayofanana, hivyo itachukua muda 'kidogo' kurekebisha mapungufu hayo na si jambo linalotatulika kwa haraka.

"Tatizo kubwa linalowakabili wachezaji wangu ni kukosa utimamu wa mwili na pumzi, hivyo wanachoka mapema hawawezi kumaliza dakika 90 kwa nguvu na kasi ile ile, na hili linatatulika kwa kunipa muda, japo siwezi kusema nitalitibu kwa muda gani, labda wiki tatu au zaidi nitaweza kulitatua," alisema Ramovic.

Kocha huyo alisema kipindi cha kwanza timu yake ilitawala mchezo wakapata nafasi za kufunga na endapo wangefanikiwa kupata mabao, hadhithi ingekuwa nyingine.

"Kipindi cha kwanza tulitawala mpira tukapata nafasi lakini hatukufunga, kuna nafasi ilitokea kama Stephane Aziz Ki angefunga, ingewezekana mambo yangekuwa tofauti.

Hata hivyo, tuna michezo mitano imebaki, safari bado ni ndefu katika kundi hili, tunakwenda kufanyia kazi mapungufu ili tushinde michezo inayokuja," Ramovic alisema.

Naye Kocha Mkuu wa Al Hilal, Florent Ibenge, amefurahishwa na ushindi huo wa ugenini, ingawa alisema haukuwa ushindi rahisi kutokana na ubora wa Yanga.

"Hatukuanza mchezo vizuri, hatukuwa tunamiliki mpira, tulikuwa tunapoteza mipira mingi, nafikiri mwanzoni walipata nafasi mbili za uwezekano wa kufunga lakini baada ya hapo tukamudu kuzuia, baadaye tukafunga mabao mawili yaliyokuwa muhimu kwetu.

Niliwaambia viungo na mabeki wangu wasiwape sana nafasi ya kukaa na mpira na wasikae nao mbali sana na hilo lilisaidia sana kwa sababu wachezaji wao kabla hajafikiria nini cha kufanya, vijana wangu tayari walikuwa wameshafika na kutibua mipango," Ibenge alisema.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga kushika mkia katika Kundi A baada ya TP Mazembe kulazimishwa suluhu ikiwa nyumbani dhidi ya MC Alger wakati Al Hilal ikiakaa kileleni na pointi tatu kibindoni.