Mgombea, Wakala CHADEMA mbaroni madai ya kutimka na sanduku la kura

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 07:35 PM Nov 27 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa.
Picha:Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa.

JESHI la Polisi mkoani Mwanza linawashikilia makada wanne wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo wizi wa sanduku la kura lenye karatasi 181 pamoja na kufanya vurugu katika kituo cha kupigia kura.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa, amethibitisha kukamatwa kwa makada hao leo Novemba 27, 2024 ambao ni Mgombea nafasi ya Mwenyeki katika Mtaa wa Maliza jijini Mwanza, Athanas Ndaki, Katibu wa chama hicho Wilaya Boneface Ntobi, pamoja na Mawakala wawili wa kituo cha Lwanima ‘A’ Ally Hussein na Lwanima ‘B’ Edward Otieno.

DCP Mutafungwa amesema mgombea pamoja na mawakala wawili wanashikiliwa kwa tuhuma za kukimbia na box la kura lilikuwa na karatasi 181 ambazo tayari zimepigiwa kura kutoka katika Kituo cha Lwanima ‘B’.

“Tukio hili limetokea majira ya saa 4:30 asubuhi katika kituo cha kupigia kura cha Lwanima ‘B’, Mtaa wa Maliza ambako Wakala wa chama hicho Otieno aliyekuwa katika kituo hicho alianza mawasiliano na Mgombea wa Mtaa kupitia chama hicho Athanas Ndaki ambaye alifika kwenye kituo na katika hali ya kushangaza wakala huyo alichukua box la karatasi za kupigia kura na kuondoka nazo akiungana na mgombea huyo,” amesema DCP Mutafungwa.

Aidha amesema baada ya tukio hilo Askari wa jeshi la akiba aliyekuwa anasimamia kituo hicho alianza kumfukuza na kutoa taarifa kwa askari polisi ambao walishirikiana na kumkamata Wakala huyo pamoja na Mgombea na Wakara wa Kituo jirani cha Lwanima ‘A’ wakiwa na karatasi hizo za kupigia kura.

Kamanda Mutafungwa amesema pia wanamshikilia Katibu wa Chadema Wilaya, Boneface Ntobi  kwa kufanya fujo katika kituo cha kupigia kura cha Kabengo kilichopo Mtaa wa Mabatini Wilaya ya Nyamagana.

“Alikuwa akifanya vurugu akidai kwamba kituo hicho hakipo kwenye orodha ya vituo vya kupiga kura katika Mtaa huo,”amesema DCP Mutafungwa