Tamasha la Chakula la Coca-Cola Tanzania, maarufu kama Kitaa Food Fest, limehitimishwa kwa kishindo jijini Dar es Salaam, likiangazia ubunifu katika upishi wa vyakula vya asili ya Kitanzania sambamba na matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Tukio hilo lililofanyika Novemba 23, katika viwanja vya 710 Kawe, Dar es Salaam liliwakutanisha zaidi ya Mama na Baba Lishe 40 wa Kitanzania, ambao walionyesha uwezo wao wa kuandaa vyakula vya asili vilivyozingatia utunzaji wa mazingira na afya.
Meneja Mwandamizi wa Masoko wa Coca-Cola Tanzania, Kabula Nshimo, amesema:"Ubunifu wa wapishi wa Kitanzania, pamoja na dhamira ya kutumia nishati safi ya kupikia, umefanya tamasha hili kuwa kivutio cha kipekee. Ni fahari kuona tunasherehekea vyakula vya asili huku tukihamasisha matumizi ya mbinu endelevu," amesema Kabula.
Tamasha hilo pia lilihusisha mbinu za kisasa za upishi zilizowasilishwa na mpishi maarufu kutoka Kenya, Dennis Ombachi, anayejulikana kama The Roaming Chef. Ombachi alifundisha umuhimu wa kutumia vifaa vya kisasa na nishati salama katika upishi wa vyakula vya asili.
Mbali na chakula, tamasha hilo lilitoa burudani za muziki kutoka kwa wasanii wa hapa nchini, likisisitiza mshikamano wa kijamii.
Kaimu Meneja Mkuu wa Coca-Cola Kwanza, Jonathan Jooste, amesema kuwa:"Tamasha hili linaonyesha jinsi chakula, burudani, na vinywaji vya Coca-Cola vinavyoweza kuunganisha watu huku tukihamasisha utunzaji wa mazingira,” amesema Jooster.
Kitaa Food Fest ni jukwaa linaloonyesha jinsi vyakula vya asili vinaweza kuendana na nishati safi na mbinu za kisasa.
Tukio hilo ambalo lilihudhuriwa na zaidi ya wakazi 300 wa Dar es Salaam limeacha alama kubwa katika kukuza utamaduni na ubunifu wa Kitanzania kwa njia endelevu.
Baadhi ya vyakula vylivyopikwa katika tamasha hilo ni ugali samaki, wali, pilau, ndizi nyama, kuku wa kuchoma, kisanvu, mhogo, kisamvu na vingine vingi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED