Ndugulile afariki dunia kabla kukalia kiti chake kipya WHO

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 10:13 AM Nov 28 2024
MBUNGE wa Kigamboni ambaye pia ni Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dk. Faustine Ndugulile, amefariki dunia India.
Picha:Mtandao
MBUNGE wa Kigamboni ambaye pia ni Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dk. Faustine Ndugulile, amefariki dunia India.

MBUNGE wa Kigamboni ambaye pia ni Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dk. Faustine Ndugulile, amefariki dunia India alikokuwa anapatiwa matibabu.

Rais Samia Suluhu Hassan, Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, WHO na wadau kwa nyakati tofauti jana, walieleza masikitiko yao kumpoteza kiongozi huyo ambaye amekuwa na mchango mkubwa katika sekta mbalimbali, ikiwamo afya.

Rais Samia alisema, "Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Dk. Ndugulile, na kutoa salamu za pole kwa familia, Spika wa Bunge, wabunge, wananchi wa Kigamboni, ndugu, jamaa, marafiki na watanzania wote.

Spika wa Bunge, Dk. Tulia alisema kifo cha Dk. Ndugulile kilichotokea usiku wa kuamkia jana, kimeacha simanzi kubwa kwa Bunge na watanzania kwa ujumla kutokana na mchango wake mkubwa katika maendeleo ya taifa.

Akizungumza jana mara baada ya kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, huko mtaa wa Uzunguni A, jijini Mbeya, Spika Tulia alisema nyota ya Dk. Ndugulile imezimika wakati akiwa ameanza kung’ara katika anga za kimataifa.

"Misiba yote ni migumu lakini kwa msiba huu ni mgumu zaidi kwa sababu pamoja na kwamba alikuwa mbunge, alikuwa mtu ambaye dunia imeshamwamini, ukiacha nafasi mbalimbali hapa nchini alizowahi kuzifanyia kazi.

"Alikuwa ameshaaminiwa kutuwakilisha kuwa Mkurugenzi mkubwa WHO Kanda ya Afrika. Wote tulishiriki kwa maombi na Mheshimiwa Rais alishiriki kwa maombi kuhakikisha nafasi hii inakuja Tanzania, sasa mipango ya mwanadamu na Mungu ni tofauti," alisema.

Dk. Tulia alisema Dk. Ndugulile pia ametoa mchango katika eneo la afya na kwa kipindi hiki alikuwa Makamu Mwenyekiti Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, ambapo kuna sera zimebadilika na sheria zimetungwa kwa sababu ya michango yake.

"Mimi ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, kule nako alikuwa anaongoza kundi linaloshughulikia masuala ya afya. Mchango wake katika sekta ya afya ni mkubwa, ni mmoja wa viongozi ambao tumewapoteza kipindi ambacho tunawahitaji zaidi," alisema Dk. Tulia.

Taarifa iliyotolewa jana na Kitengo cha Mawasiliano na Elimu kwa Umma, Ofisi ya Bunge, ilisema Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na familia wanaendelea kuratibu shughuli za mazishi na taarifa zaidi zitatolewa.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO), Dk. Tedros Adhanom Ghebreyesus kupitia mtandao wa X jana aliandika:

"Nimeshtushwa na kusikitishwa sana na taarifa za msiba wa ghafla wa Dk. Faustine Ndugulile, Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (Kanda ya Afrika), Salamu zangu za rambirambi kwa familia, Bunge na wananchi wa Tanzania."

CCM YAMLILIA

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla, alisema wameshtushwa kwa sababu Dk. Ndugulile alikuwa akiwakilisha Tanzania duniani.

"Alikuwa kada wa CCM na mwanachama mwaminifu, ametumikia unaibu waziri na uwaziri. Ni pigo kubwa kwa Tanzania na dunia aliyokuwa anakwenda kwenye nafasi ya Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika, tumepoteza mtu makini na mwenye weledi, mzalendo. CCM inamlilia," alisema.

Makalla ambaye pia ni Mlezi wa Mkoa wa Dar es Salaam, alisema, Dk. Ndugulile ametoka Tanzania akiwa bado ni mbunge, alikuwa anapenda wananchi wake na alikuwa kiongozi mfuatiliaji.

Godbless Lema, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Kaskazini, alisema jana kuwa, "maisha haya tunapita haraka kama upepo. Kuishi kwa mema ni jukumu la msingi kabisa katika maisha.

"Hata sijui kwa nini binadamu tunakuwa na viburi. Nilimfahamu Dk. Ndugulile tukiwa bungeni. Nimeshtuka kusikia amefariki dunia, jipeni moyo sana familia, ndugu, jamaa na marafiki."

KAULI YAKE BUNGENI

Septemba 3 mwaka huu, wakati akitoa shukrani bungeni, Dodoma, Dk. Ndugulile alisema: "Niwaombe mniombee, tuendeleze sala na dua nyingi, kwani nafasi hii imebeba maono ya watanzania na waafrika wanatarajia makubwa."

Dk. Ndugulile ni mtanzania wa kwanza na mwana Afrika Mashariki wa kwanza kuteuliwa kushika nafasi hiyo nyeti WHO. Na kituo chake cha kazi kilikuwa ni Congo Brazzavile.

Machi 27 mwaka huu, alipata ushindi huo baada ya nchi 19 kuipigia kura Tanzania katika mzunguko wa kwanza, 12 wakiipigia Senegal, saba Niger na nchi saba zikiipigia Rwanda. Matokeo yalitangazwa siku hiyo katika Mkutano wa Afya wa 78 wa WHO uliofanyika Congo Brazzaville.

Katika mzunguko wa pili wa uchaguzi, alipata kura 25, Senegal 14 na Niger kura sita. Dk. Ndugulile alipigiwa kura na mawaziri wa afya kutoka nchi za Afrika.

Machi 11, 2023, aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Ushauri Masuala ya Afya ya Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), akiwa sehemu ya wabunge 12 wanaoshauri IPU masuala ya afya, uteuzi ulioanza Februari mwaka huo.

Nafasi nyingine ambazo amewahi kuhudumu ni pamoja na Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Uchunguzi Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii (2004-2006), Waziri wa Mawasiliano na Tekonolijia ya Habari (2020-2021) na Naibu Waziri Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (2017-2020).

Mwaka 1997-1998, Dk. Ndugulile alikuwa daktari katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na alikuwa mtaalamu wa maikrobaiolojia hadi mwaka 2004 alipoteuliwa kuwa Meneja wa Programu Wizara ya Afya.

Mwaka 2004-2006, alihudumu kama Mkuu wa Kitengo cha Uchunguzi wizarani huko na mwaka 2007-2010 alikuwa Mshauri wa Afya katika Taasisi ya Udhibiti wa Magonjwa (CDC) Afrika Kusini. Kati ya mwaka 2006 na 2007 alihudumu kama Meneja Program katika Mpango wa Damu Salama.

ELIMU

Dk. Ndugulile alizaliwa Machi 31, 1969, wilayani Mbulu, mkoani Manyara. Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Groombridge iliyoko Harare, Zimbabwe kuanzia mwaka 1976 na kuhitimu 1982.

Mwaka 1982-1986 alipata elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Prince Edward, Harare na baada ya kufaulu, aliendelea na elimu ya kidato cha tano na sita katika Shule ya Tambaza iliyoko Dar es Salaam (mwaka 1987-1989).

Mwaka 1990-1997 alisomea shahada ya kwanza ya udaktari (MD) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na baadaye akachukua shahada ya uzamili (MMED) chuoni huko alikohitimu mwaka 2001.

Kukiwa na msiba huo wa kimataifa, Mchumi na Mwanataaluma Mbobezi, Dk. Oswald Mashindano, alifariki dunia usiku wa kuamkia jana na msiba uko nyumbani kwake, Kijichi, Dar es Salaam.

Dk. Mashindano aliwahi kuwa Msajili wa Hazina, Mhadhiri Mwandamizi UDSM Idara ya Uchumi na Mtafiti Mwandamizi Mshiriki wa Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Uchumi na Jamii (ESRF).