VITA ya kuwania pointi tatu muhimu inatarajiwa kuendelea leo kwa wenyeji Azam FC kuwakaribisha Singida Black Stars katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Azam na Singida Black Stars zitakutana kila moja ikiwa na pointi 24 kibindoni baada ya kucheza michezo 11 sawa na vinara Simba yenye pointi 28.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Azam FC, Rachid Taoussi, alisema wachezaji wake wako tayari kwa mchezo huo na wanaamini wataingia kupambana kuhakikisha wanapata ushindi.
Taoussi alisema wamejiandaa kukutana na ushindani kwa sababu wapinzani wao wamekuwa na kiwango bora na wanarekodi nzuri katika michezo iliyotangulia.
"Tuko tayari kwa ajili ya mechi hii, tunaendelea kupambana kuhakikisha tunapata ushindi, malengo yetu ni kutwaa ubingwa na kushiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani," alisema kocha huyo.
Kaimu Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, Ramadhani Nsanzurwimo, alisema wamejipanga kucheza soka la ushindani kwa sababu wanakutana na timu yenye wachezaji 'wakubwa' na wenye uzoefu katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Nsanzurwimo alisema kila mechi kwao ni sawa na fainali na malengo yao ni kupata ushindi na si matokeo mengine.
"Tunajua mechi itakuwa ngumu, Azam wanataka kwenda juu na sisi tunataka kubaki hapo hapo, tunatarajia watu watashuhudia mechi nzuri na yenye ushindani, ni mechi kubwa, lengo letu ni kupata pointi tatu muhimu," alisema Nsanzurwimo.
Aliongeza hakuna mechi rahisi katika Ligi Kuu msimu huu kwa sababu timu zote zimejiimarisha kupata matokeo chanya na si kusindikiza wengine.
"Kila siku tunapokutana na Azam inakuwa ni mechi nzuri na mechi ya kupendeza. Wao wana timu nzuri na sisi tunatimu nzuri, hatujaja kutembea hapa Dar es Salaam, tumekuja kutafuta pointi tatu," alisema kocha huyo.
Alisema pia kikosi chake hakijatetereka kutokana na kutimuliwa kwa aliyekuwa Kocha Mkuu, Patrick Aussems, kwa sababu yeye (Nsanzurwimo) na wengine walikuwapo katika benchi la ufundi, hivyo wataendeleza mazuri yaliyopo.
Naye nyota wa Singida Black Stars, Ayubu Lyanga, alisema wamejiandaa vizuri kuondoka na ushindi katika mechi hiyo na yaliyotokea katika mchezo uliopita yameshaondoka kwenye akili zao.
Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajia kuendelea tena kesho kwa KMC kuwaalika Tabora United wakati Fountain Gate itacheza dhidi ya JKT Tanzania na keshokutwa Namungo itawakaribisha Yanga kwenye Uwanja wa Majaliwa ulioko Ruangwa mkoani Lindi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED