Pamba Jiji yajipanga kurudi kivingine mzunguko wa pili

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:17 AM Jan 02 2025
Msemaji wa Timu ya Pamba Jiji, Moses William
Picha: Mtandao
Msemaji wa Timu ya Pamba Jiji, Moses William

KLABU ya Pamba Jiji imesema kuelekea mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, inaendelea kujipanga na kufanya usajili wa uhakika ili kurejea na makali kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.

Meneja wa timu hiyo, Ezekiel Ntibikeha, alisema mbali na wachezaji iliyowasajili ambao tayari wameshaanza kuonekana kwenye baadhi ya michezo, wanaendelea na usajili mkubwa wa wachezaji ambao watakibadilisha kikosi chao kuwa imara.

"Tulitegemea walau mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu tuwe na pointi 20, lakini tumemaliza na pointi 12, tumeanza na tunaendelea kufanya maboresho makubwa kwa sababu tumeiona ligi ilivyo inahitaji watu wa aina gani, mpaka kufungwa kwa dirisha dogo tutakuwa tayari tumeshamaliza kujaza mapengo maeneo ambayo tunahisi yalihitaji marekebisho," alisema meneja huyo.

Aidha, aliwataka mashabiki wa soka jijini Mwanza kutokata tamaa, badala yake kuiunga mkono timu hiyo ili itimize lengo lake kuu kwa msimu huu ambalo ni kubaki Ligi Kuu.

"Mashabiki wa Mwanza wanatakiwa kutuunga mkono, sisi tutahakikisha tunasajili wachezaji mahiri ambao wanaweza kuitoa timu hapa ilipo na kuipeleka sehemu nyingine, na niziambie tu tumu zingine zisikariri, zisitarajie kukutana na Pamba hii ya mzunguko wa kwanza, badala yake watakutana na nyingine kabisa ambayo imeboreshwa," alisema.

Tayari kutoka timu hiyo inaeleza mpaka sasa imeshawasajili Zabona Mayombya kutoka Prisons, Cherif Ibrahim beki wa kushoto kutoka Coton Sport ya Cameroon, Hamad Majimengi, Habib Kyombo, Deus Kaseke, pamoja na kipa Mohamed Kamara raia na Sierra Leone, ambaye ametua kwenye kikosi hicho kwa mkopo akitokea Singida Black Stars.

Timu hiyo ambayo mpaka sasa imecheza michezo 16, ipo kwenye nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 12.