WACHEZAJI wakongwe wa klabu ya Simba, Nahodha Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr' na Shomari Kapombe, wamesema wamejiandaa kuhakikisha wanarejesha heshima klabuni hapo baada ya kutoka kapa kwenye ubingwa kwa misimu mitatu mfululizo.
Wakizungumza na gazeti hili jana, nyota hao wamesema usajili uliofanywa na viongozi wao umerejesha makali ya klabu hiyo kutokana na ubora wa wachezaji.
"Tumefanya maandalizi mazuri kambini, wachezaji wapya waliosajiliwa wameonyesha wana uwezo mkubwa pamoja kwa kushirikiana tunataka kurejesha heshima ya Simba kwa kutwaa ubingwa na kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya kimataifa," alisema Zimbwe Jr.
Alisema benchi la ufundi la timu hiyo chini ya kocha Fadlu David, wamewapa mbinu mbalimbali na mipango ya kuhakikisha wanafanya vizuri.
"Tuna mchezo wa kirafiki Siku ya Simba Day, lakini tuna mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, ni michezo ambayo itatupa mwanga wa kuanza vizuri msimu huu, tumejiandaa vizuri," alisema Zimbwe.
Aidha, Kapombe, aliwataka mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi siku ya tamasha la 'Simba Day' ili kuwaona wachezaji wao wapya.
"Msimu huu tunataka uwe wetu, viongozi wamefanya kazi kubwa na sasa ni sisi wachezaji, mashabiki waje kwa wingi kama kawaida yao kuona wachezaji wao," alisema Kapombe.
Tamasha la Simba Day limepangwa kufanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo Simba itacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya APR ya Rwanda.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED