NBC yaipamba Mzizima Derby Zanzibar, yakabidhi tuzo, fedha kwa mchezaji, kocha bora wa Agosti

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:25 PM Sep 27 2024
Mwenyekiti wa Chama Cha Soka Mkoa wa Dar Es Salaam (DRFA) Lameck Nyambaya (Kushoto) akikabidhi hundi yenye thamani ya sh milioni moja  kwa kocha mkuu wa klabu ya SC Fadlu Davids alietangazwa kocha Bora wa Ligi Kuu ya NBC kwa mwezi Agosti.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mwenyekiti wa Chama Cha Soka Mkoa wa Dar Es Salaam (DRFA) Lameck Nyambaya (Kushoto) akikabidhi hundi yenye thamani ya sh milioni moja kwa kocha mkuu wa klabu ya SC Fadlu Davids alietangazwa kocha Bora wa Ligi Kuu ya NBC kwa mwezi Agosti.

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), mdhamini Mkuu wa Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara, NBC Premiere League jana iliipamba mechi kati ya Azam FC na Simba SC maarufu kama ‘Mzizima Derby’ kwa kuandaa matukio kadhaa ikiwemo kukabidhi zawadi ya tuzo na pesa taslimu kwa mchezaji na kocha bora wa ligi hiyo kwa mwezi Agosti.

Mchezo huo ulifanyika kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar na kuisha kwa timu ya Simba SC kuibuka na ushindi wa goli 2-0. Wateja mbalimbali wa benki ya NBC walipata fursa ya kuutazama mchezo huo wakiwa katika jukwaa la VIP kupitia udhamini wa benki hiyo.

Meneja wa Benki ya NBC tawi la Zanzibar, Abdul Karim Mkila aliiwakilisha benki hiyo katika kukabidhi tuzo na hundi ya fedha yenye thamani ya Sh.milioni moja, kwa mchezaji bora mwezi Agosti, ambae ni kiungo wa Simba SC, Jean Charles Ahoua huku Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) Lameck Nyambaya akikabidhi zawadi kama hizo kwa K0cha Mkuu wa Klabu ya SC Fadlu Davids ambae aliiibuka kocha bora kwa mwezi huo.

Katika mchezo huo wa jana ilishuhudiwa kipa wa Simba SC, Moussa Camara akiibuka mchezaji bora wa mchezo huo na kukabidhiwa zawadi ya tuzo kutoka benki hiyo.