Morocco kukata rufaa adhabu ya CAF

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:50 PM Feb 05 2026
news
Picha Mtandao
Morocco kukata rufaa adhabu ya CAF

SHIRIKISHO la mpira wa miguu la Morocco, FRMF, limesema litakata rufaa dhidi ya adhabu za kinidhamu na faini zilizotolewa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), baada ya matukio ya vurugu kwenye fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON 2025, dhidi ya Senegal mwezi uliopita.

Morocco ilitozwa faini ya jumla ya dola 315,000 mwezi uliopita, na kuwafungia wachezaji wake wawili.

Katika taarifa ya FRMF ilisema itakata rufaa "ili kulinda haki zote zilizohakikishwa na kanuni", ikitaja "kutofuata adhabu hizo kwa kiwango na uzito wa matukio yaliyotokea".

Fainali ya AFCON mnamo Januari 18 ilikuwa na mfululizo wa matukio ya utovu wa nidhamu, baada ya bao la Ismaila Sarr kukataliwa kwa madai ya kumchezea faulo mchezaji bora wa mwaka wa Afrika wa 2025, Achraf Hakimi.

Kisha Morocco ilipewa penalti wakati Brahim Diaz alipofanyiwa madhambi, na Senegal ikatoa timu uwanjani.

Morocco ilikosa penalti hiyo iliyocheleweshwa kwa muda mrefu kwa shuti dhaifu kutoka kwa Diaz lililookolewa na Edouard Mendy. 

Mechi hiyo ilienda kwenye muda wa ziada na Pape Gueye akafunga na kuipa Senegal taji la pili la AFCON.

Morocco ilitozwa faini ya dola 200,000 kwa "tabia isiyofaa kwenye uwanja wa mpira".

Faini nyingine ya dola 100,000 ilitozwa kwa "tabia isiyofaa" ya kumfuata mwamuzi kwenye ukaguzi wa VAR.

Pia na faini ya dola 15,000 ni baada ya mashabiki wa Morocco kuwafanyia vurugu wale wa Senegal.