Mo: Kibu hauzwi, Simba ikiwaandalia dozi Fountain Gate

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:40 AM Feb 06 2025
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids
PIcha: Mtandao
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids

IKITARAJIWA kuwakabili wenyeji Fountain Gate FC katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa ulioko Babati mkoani Manyara, Wekundu wa Msimbazi wamekataa kumuuza nyota wao, Denis Kibu, kwa MC Algers ya Algeria, imefahamika.

Mechi ya leo itakuwa ni mchezo wa tisa kwa Simba kushuka nje ya uwanja wake wa nyumbani, ambapo katika michezo nane imepata ushindi wa asilimia 100.

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, aliliambia gazeti hili, timu yake imejipanga kuondoka na pointi tatu muhimu ili kuendeleza kutoa dozi katika kila inapocheza ugenini msimu huu.

Kocha huyo alisema Simba imekuwa na matokeo mazuri inapocheza ugenini na hii inachagizwa na idadi kubwa ya mashabiki wanaojitokeza viwanjani kuwashangilia wachezaji wao.

"Nilisema na narudia tena, tunashinda sana ugenini kwa sababu tunacheza mechi za mikoani kama tupo nyumbani kutokana na kushangiliwa na mashabiki wengi zaidi kuliko wapinzani wetu ambao ni wenyeji, natarajia mechi hii itakuwa hivyo hivyo, na sisi tutawapa na kuwaachia mashabiki furaha ya ushindi, tukichukua pointi tatu na kurejea nazo Dar es Salaam," alisema Fadlu.

Hata hivyo, Simba inaweza kumkosa winga wake tegemeo, Kibu, aliyeumia katika mchezo uliopita, ingawa daktari wa timu, Edwin Kagoba, amesema hali yake inaendelea vizuri.

"Yuko katika hatua ya pili ya matibabu, tunategemea, atakapopita kwenye hatua zote za matibabu anaweza kuwapo kwenye mchezo wetu ujao. Ila hii uwepo wake ni nusu kwa nusu, kuna vitu tunaviangalia leo (jana) na kesho (leo), lakini niwatoe hofu wanachama na mashabiki wa Simba hali yake si mbaya si ya kumweka nje muda mrefu," alisema daktari huyo.

Naye Kocha Mkuu wa Fountain Gate, raia wa Kenya, Robert Matano, amesema  amekiandaa vyema kikosi chake kushindana na Simba, ingawa anaamini watawapa upinzani mkali.

"Ninataka kushinda, najua utakuwa mchezo wa kwanza kwangu tangu niichukue timu, hapa siwezi kueleza sana siri zangu za vita, subirini dakika 90," alisema Matano.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohamed Dewji 'Mo', amesema klabu hiyo haiko tayari kumuuza Kibu kwa sababu inapambana kuwania taji la Ligi Kuu na inahitaji kufanya vyema katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.