BAADA ya kuishuhudia timu ya Simba ikishindwa kufikia malengo yake ya kutinga hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, rais wa Heshima na Mwekezaji wa klabu hiyo, Mohamed 'Mo' Dewji, amesema mwishoni mwa msimu atakutana na Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha, kwa ajili ya kufanya tathimini ya kina na kukifanyia maboresho makubwa kikosi hicho.
Simba wametupwa nje katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly, kwa jumla ya mabao 3-0 katika michezo yote miwili nyumbani ikiruhusu bao 1-0 na kisha ugenini nchini Misri, kukubali kichapo cha mabao 2-0.
Hata hivyo, jana Mo Dewji alisema ameziangalia mechi zote na ameona jinsi gani wachezaji walivyopambana na anaimani na utendaji kazi mzuri wa benchi la ufundi , hivyo anatarajia kukutana na kocha kwa ajili ya kuangalia mapungufu ya timu yao na kufanya maboresho.
Alisema watafanya maboresho kulingana na mahitaji ya kocha Benchikha, kwa ajili ya kuimarisha kikosi cha timu hiyo kwa kuleta wachezaji wenye uzoefu mkubwa wa kuwatoa hatua waliyofikia na kusonga mbele katika michuano ya kimataifa.
“Naipenda Simba sana, inapofanya vibaya naumia, tumefanikiwa kucheza robo fainali mara nyingi, tutafanya mabadiliko mwishoni mwa msimu huu kuboresha kikosi chetu kwa kuleta wachezaji wenye uzoefu kwa kuzingatia mapendekezo ya benchi la ufundi,” alisema Mo Dewji.
Aliongeza kuwa matarajio yake makubwa ni kufanya maboresho kwa msimu ujao ili waweze kufikia malengo yao, akiamini kuwa hatua ya kufika nusu fainali itakuwa taratibu kama ilivyo kwa hapo awali kwani hakuna mtu ambaye anaamini Simba ingecheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika hatua nyingine, Simba leo itashuka katika Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma kuvaana na Mashujaa FC, kwenye mechi ya 16-bora ya CRDB Federation Cup.
Simba itashuka uwanjani ikiwa na kazi ya kutaka kuwafariji wanachama na mashabiki wa timu hiyo ambao wanaonekana kuhuzunika kwa kuchapwa mabao 2-0 dhidi ya Al Ahly ya Misri kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, katika mechi iliyochezwa Ijumaa iliyopita Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, ikisukumwa nje kwa jumla ya mabao 3-0, kutokana na kufungwa bao 1-0 nyumbani.
Kutokana na kuondolewa kwa michuano hiyo, Simba imebakisha mataji mawili ambayo inaendea kupambana nayo kwa ajili kuyatia kibindoni nayo ni kombe hilo pamoja na Ligi Kuu Tanzania Bara, huku ikiwa tayari ina Ngao ya Jamii mkononi iliyoitwaa Agosti 13, ilipowachapa watani zao wa jadi, Yanga kwa mikwaju ya penalti 3-1, mechi iliyochezwa Agosti 13, mwaka jana, Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Simba inakwenda kucheza na timu ambayo mara mwisho ndiyo iliyokutana nayo katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, Machi 15, na kushinda mabao 2-0.
Timu yoyote itakayoshinda itatinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ambayo bingwa wake huiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Kocha Mkuu wa Simba, Benchikha amesema wanakwenda kucheza mechi hiyo muda mfupi tu baada ya kutoka mechi yao dhidi ya Al Ahly tena wakiwa ugenini, hivyo anatarajia kutakuwa na uchovu kwa wachezaji wake, lakini hiyo haiwezi kuwa kisingizio cha kutofanya vizuri kwenye mchezo wa leo.
"Tuna baadhi ya wachezaji ambao hawakucheza mechi ile tutawatumia, lakini pia wapo waliocheza ila watatumika kwa dakika kadhaa au zote kutegemea na mwenendo wa mechi," alisema
Kocha Mkuu wa Mashujaa, Mohamed Abdallah 'Bares', amesema kutokana na mazoezi ambayo amewafanyisha vijana wake, anaamini watafanya vizuri katika mechi ya leo.
"Tumekaa muda mrefu bila kucheza mechi yoyote, nadhani mara ya mwisho tulicheza dhidi ya hawa hawa Simba, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu, tuliwapa mapumziko mafupi wachezaji wetu, lakini walirejea na kufanya mazoezi ya nguvu kujiandaa na mchezo huu, naamini tutafanya vizuri," alisema kocha huyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED