WAKATI Klabu ya Simba ikikamilisha usajili wa wachezaji wapya kwa kumtangaza kiungo mkabaji kutoka Singida Black Stars, Yusuph Kagoma huku mlinda lango wao raia wa Morocco, Ayoub Lakred, akisaini mkataba mpya wa mwaka mmoja, Mwekezaji, rais wa Heshima na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohamed 'Mo' Dewji, amesema ameamua kufanya usajili wa nguvu ili kurejesha heshima ya klabu hiyo.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mo alisema amefanya usajili huo mkubwa kwa kuwashirikisha wataalam zaidi ya 50 kutoka nchi mbalimbali duniani, ikiwamo Tanzania.
"Naamini tumefanya usajili mkubwa na mzuri, haikuwa kazi rahisi, nimejaribu kuwasiliana na watu zaidi ya 50 kwa ajili ya usajili huu, nilishirikiana na maskauti kutoka nchi za Uholanzi, Ufaransa, na wengine hapa Tanzania kuweza kusajili wachezaji hawa.
"Kama mnavyoona timu safari hii ina vijana wengi sana, wanaanzia miaka 20 hadi 24 hivi, kwa hiyo nina imani kubwa tukienda kwenye maandalizi yetu, kikosi kikawa na muunganiko mzuri, watatuletea matokeo mazuri na kurudisha furaha yetu," alisema mwekazaji huyo.
Mo, alisema amefurahi kukutana na kuwaona wachezaji ambao amewasajili na wengineo, kwani wengi wao ni mara ya kwanza kukutana nao 'laivu'.
"Nimefurahi kwani, wachezaji wengi wametoka nchi mbalimbali, ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kukutana nao, pia nimepata bahati ya kukutana na kocha mkuu, benchi la ufundi, tulikuwa na mazungumzo mazuri, timu sasa inaanza kwenda Misri ya kwa ajili ya 'pre season', tutakaa pale siku kama 20 hivi, Mungu akitujalia tutarudi mwisho wa mwezi huu kwa ajili ya Simba Day, Agosti 3," alisema Mo.
Jana mchana, klabu hiyo ilimtangaza kiungo mkabaji, Kagoma, akisajiliwa kwa mkataba wa miaka mitatu kutokea, Singida Big Stars.
Kabla ya hapo, aliwahi kuichezea Klabu ya Geita Gold kisha kujiunga na Singida Fountain Gate, ambapo baadaye alikwenda Ihefu FC, ambayo imebadilishwa jina la kuitwa Singida Black Stars.
Kusajiliwa kwa mchezaji huyo kunafanya Simba iwe na wachezaji 12 wapya iliyowasajili kuelekea msimu ujao, saba wakiwa wageni na watano wazawa.
Wachezaji saba wa kigeni ni Jushua Mutale kutoka Power Dynamos ya Zambia, Steven Mukwala akitokea Asante Kotoko ya Ghana, Jean Charles Ahoa kutoka, Stella Adjame ya Ivory Coast, Debora Fernandes Mavambo kutoka Mutondo Stars ya Zambia, Augustine Okajepha, kutoka Rivers United ya Nigeria na Karaboue Chamou, akitokea Klabu ya Racing Club d'Abidjan ya Ivory Coast.
Wachezaji wazawa waliotangazwa mpaka sasa ni Lameck Lawi kutoka Coastal Union, Abdulrazack Hamza wa Super Sports ya Afrika Kusini, Valentino Mashaka, akitokea Geita Gold, Omari Omari aliyekuwa akikipiga na Mashujaa FC na Kagoma.
Msafara wa watu 30 wakiwamo wachezaji, benchi la ufundi na wafanyakazi wengine walitarajiwa kuondoa jana nchini saa 11:00 jioni kuelekea Ismailia, Misri kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa mashindano.
Klabu hiyo imesema kuwa kipa wake namba moja, Ayoub Lakred, ndiye mchezaji pekee ambaye hajajiunga nao kwenye msafara kwani anatarajiwa kujiunga nao kambini akitokea nchini kwao, Morocco.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED