Mo afanya kikao kizito mechi Yanga, Benchikha, awaweka kitimoto wachezaji

By Adam Fungamwango ,, Saada Akida , Nipashe
Published at 08:58 AM Apr 16 2024
news
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwekezaji na Rais wa Heshima wa Klabu ya Simba, Mohamed 'Mo' Dewji.

MWEKEZAJI na Rais wa Heshima wa Klabu ya Simba, Mohamed 'Mo' Dewji, amefanya kikao kizito na Bodi ya Wakurugenzi kutokana na mwenendo mbovu wa timu hiyo, huku Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha, akiwaweka kitimoto wachezaji wake kujua tatizo lipo wapi ili kuweka mambo sawa kuelekea katika mechi ya Jumamosi wiki hii dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga.

Taarifa za uhakika zilizoifikia Nipashe jana, kutoka ndani ya Bodi ya Wakurugenzi Simba, imeeleza kuwa baada ya kuondolewa kwenye Kombe la FA, na kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Ihefu FC, viongozi, benchi la ufundi la wachezaji walikuwa na kikao cha pamoja wakiongozwa na Mo mwenyewe, ambacho lengo lake ni kujua tatizo ni nini na linaanzia wapi na namna ya kulirekebisha.

Mtoa habari anasema kulikuwa na ajenda mbili, kwanza ni kwa nini timu inashindwa kupata matokeo katika mechi zake kadhaa za hivi karibuni, lakini pia mipango ya kuelekea mchezo wa Jumamosi dhidi ya Yanga.

Mo, mwenyewe ameposti picha kwenye akaunti yake ya instagram, ambayo inaonyesha yupo kwenye kikao na baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo na kukiri kufanya hivyo, akiwataka wanachama na mashabiki wa Simba wasife moyo.

"Nimefanya kikao na viongozi wa Simba kujua changamoto zipo wapi na namna ya kuzitatua. Kikao kimeenda vizuri, Wanasimba tusife moyo, tuendele kushirikiana," aliandika rais huyo.

Habari zinasema kuwa mara baada ya kikao hicho, Benchikha naye akawa na kikao chake na wachezaji bila kuwahusisha viongozi.

"Ni kweli baada ya kikao cha bodi kikiongozwa na Mo mwenyewe, kocha alifanya kikao kingine na wachezaji wake tu bila ya kuwapo kwa kiongozi yeyote na kuzungumza nao na kuweka mipango yao kuelekea mechi dhidi ya Yanga.

Kocha hataki kupoteza mechi dhidi ya Yanga mara mbili, na amewataka wachezaji kuwa makini ikiwamo safu ya ushambuliaji na ulinzi kutowapa nafasi ya wapinzani kufika katika eneo, lakini pia amerejesha morali ya wachezaji,” kilisema chanzo hicho.

Ikumbukwe katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa Novemba 5, mwaka jana, Simba ilipata kipigo cha fedheha cha mabao 5-1, Uwanja wa Benjamin Mkapa, hivyo kumekuwa na hofu kubwa ya kupata kichapo kingine kikubwa kutokana na mwenendo usioridhisha wa timu hiyo, huku wanachama na mashabiki wake wakiwa wamekata tamaa.

Pia kilisema kuna uwezekano mkubwa timu kwenda kuweka kambi nje ya Dar es Salaam kwa ajili ya mechi hiyo.

"Timu inaweza kutoka Dar es Salaam, itakwenda kuweka kambi nje kama mipango itakaa sawa, kokote kule hata Zanzibar kama tulivyofanya wakati wa kujiandaa na Al Ahly," alisema mtoa habari wetu.

Naye Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally, alisema kazi kubwa waliyonayo sasa ni kusaka pointi tatu kwenye mechi dhidi ya Yanga.

"Tunatambua kwamba tuna mechi ngumu, hivyo tupo tayari kwa ajili ya mechi hii tunachoomba ni kwamba mashabiki wetu waendelee kutuunga mkono," alisema.

Simba imecheza mechi nne mfululizo bila kupata ushindi ambapo ilichezwa mbili ya nyumbani na ugenini dhidi ya Al Ahly ya Misri, ikiwa ni robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikifungwa bao 1-0 nyumbani, na mabao 2-0 ugenini, na ikatolewa kwenye michuano ya FA kwa mikwaju ya penalti 6-5 dhidi ya Mashujaa FC baada ya sare ya bao 1-1 dakika 90 za mchezo, kabla ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Ihefu, mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Jumamosi iliyopita.

Inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 46 kwa michezo 20 ambayo imecheza mpaka sasa.