Milner avunja rekodi mechi nyingi za EPL

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:04 PM Feb 22 2026
James Milner
Picha: Mtandao
James Milner

James Milner amevunja rekodi ya kucheza mechi nyingi zaidi katika historia ya Ligi Kuu England (EPL), baada ya kuanza katika mchezo wa Brighton dhidi ya Brentford hapo juzi na kufikisha mechi 654.

Milner alibadilishwa katika dakika ya 90 ya ushindi wa Brighton wa mabao 2-0 kule London Magharibi, akipigiwa makofi kutoka kwa mashabiki wa timu zote mbili ndani ya  Uwanja wa Gtech.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 40 alikuwa amefikia rekodi ya mechi 653, iliyowekwa na Gareth Barry wa Aston Villa, mapema mwezi huu.

Milner amezichezea kwa nyakati tofauti, Leeds United, Newcastle United, Manchester City, Liverpool na Brighton, akishinda mataji mawili ya Ligi Kuu alipokuwa Etihad na moja Merseyside chini ya Kocha, Jürgen Klopp.

"Kumekuwa na mazungumzo mengi kuhusu hilo. Kwangu mimi, yeyote anayenijua, jambo muhimu zaidi limekuwa timu," alisema Milner akiiambia BBC Radio 5 Live baada ya mchezo huo.

"Nimefurahi nimeweza kucheza leo (juzi) na natumaini watu wanaweza kuona bado naweza kuchangia timu.

"Ni idadi kubwa na ni vizuri kufikia rekodi, lakini ni fursa ya kuwapongeza watu wengi ambao wamenisaidia, familia na marafiki ambao wamekuwa nami tangu mwanzo.

"Madaktari wa viungo, wanasayansi wa michezo ambao wameniunga mkono, Sean Duggan, daktari wa viungo huko Brighton ambaye niliposhindwa kuinua mguu wangu kwa miezi sita mwaka jana alinisaidia kurudi uwanjani."

Milner amemzidi miaka saba Kocha Mkuu wa Brighton, Fabian Hürzeler.

Mbali ya Milner na Barry, wachezaji wengine waliocheza mechi nyingi ni Ryan Giggs (mechi 632), Frank Lampard (609) na David James (572) wanaunda tano bora.

Kipa wa Australia, Mark Schwarzer (544), Gary Speed (535), Emile Heskey (516), Jamie Carragher (508) na Phil Neville (505) wanakamilisha 10 bora.

Chanzo: Daily Mail