Mgunda amkubali Chasambi

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 07:01 AM May 23 2024
Ladack Chasambi.
Picha: Maktaba
Ladack Chasambi.

KAIMU Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda, amesema uwezo ulioonyeshwa na mchezaji wake, Ladack Chasambi, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Geita Gold uliochezwa ni wa hali ya juu na kumtaka nyota huyo kuendeleza makali yake ili afike mbali.

Katika mechi hiyo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-1 huku Chasambi akifunga magoli mawili.

Matokeo hayo yameifanya Simba kufikisha pointi 63 sawa na Azam FC iliyoko katika nafasi ya pili, ikipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Tanzania, mechi ikichezwa mapema juzi. 

Mgunda alisema kama mchezaji huyo ataendelea kujituma na kudumisha nidhamu anaamini atafika mbali kutokana na uwezo wake na kipaji alichonacho.

"Kila mchezaji amepambana kwa ajili ya timu, tumetoka nyuma na kupata ushindi, nawashukuru wachezaji lakini pia nimsifie Chasambi kwa namna alivyojituma, ni mchezaji mdogo lakini mwepesi kushika na kuyafanyia kazi maelekezo ya mwalimu," alisema Mgunda.

Kocha huyo aliongeza mechi mbili zilizobakia ni kama fainali kwao kwa sababu wanahitaji ushindi ili kujaribu kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Tayari Yanga imeshatangazwa mabingwa na vita iliyobakia ni ya kumaliza katika nafasi ya pili ili kupata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.