Mashabiki Simba kuangalia mechi yao Mwembeyanga

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:33 AM Jan 18 2025
Mashabiki wa Simba.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mashabiki wa Simba.

BAADA ya klabu ya Simba kufungiwa kuingiza mashabiki kwenye mchezo wao wa leo Uwanja wa Benjamin Mkapa, uongozi wa klabu hiyo umepanga kuwapeleka mashabiki katika viwanja vya Mwembeyanga kwa ajili ya kuangalia mchezo huo wa Kundi A.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema baada ya maoni mengi kutoka kwa watu mbalimbali, Simba na wadhamini wao wameamua kwenda kufunga televisheni kubwa kwenye viwanja hivyo vilivyoko maeneo ya Temeke jijini Dar es Salaam ili kuwapa nafasi wanachama na mashabiki waliokuwa wanataka kwenda kuangalia mchezo huo Uwanja wa Benjamin Mkapa, kwenda kwenye viwanja hivyo kwa ajili ya kuishuhudia timu yao.

"Kwa kuwa watu wana maumivu makubwa, na wanachama na mashabiki wa Simba wamezoea kukaa pamoja kijamaa kwa ajili ya kuangalia mpira, sisi na wadhamini wetu tumetenga eneo maalum ambalo wanachama na mashabiki wa Simba watakwenda kuangalia mechi hiyo dhidi ya CS Constantine, eneo tulilolipanga ni Temeke Mwembeyanga.

Tutakuwapo kuanzia saa 5:00 asubuhi, tutakuwa na TV kubwa sana, tutakuwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali," alisema Ahmed.

Alisema awali kulikuwa na mapendekezo kuwa ifungwe TV kubwa, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam ili mashabiki wakutane hapo na watakapokuwa wanashangilia kelele zao ziwafikie wachezaji na kuwatia moyo, lakini hiyo yote hairuhusiwi na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

"Awali kulikuwa na maoni mengi kuwa tuweke televisheni kubwa Uwanja wa Uhuru, ili kelele za mashabiki zikipigwa ziweze kuwafikia wachezaji, ukweli ni kwamba hairuhusiwi mita 1,000 kutoka uwanja wa mechi kuwa na shughuli za kimichezo katika eneo hilo, kwa hiyo mawazo na maoni hayo hayawezekani na tukifanya hivyo tunaweza kuadhibiwa tena.

Wengine walishauri mashabiki wasimame barabarani hadi uwanjani ili wachezaji wakipita wapigiwe makofi, hiyo nayo hairuhusiwi, tunawaomba wanachama na mashabiki wa Simba wakae mbali na Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili, kwa sababu macho ya waangalizi yatakuwa hapo, mechi ikiisha, kuanzia robo fainali mfumo wa maisha yetu utaendelea kama kawaida," alitahadharisha.

CAF, iliifungia Simba kuingiza mashabiki kwenye mchezo huo, baada ya vurugu zilizotokea Desemba 15 mwaka jana kati ya timu hiyo dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia ambapo ilishinda mabao 2-1.

Katika mchezo huo, mashabiki wa Simba na CS Sfaxien, walipigana na kusababisha viti kadhaa kung'olewa.

Akiuzungumzia mchezo huo, alisema ni muhimu kwao kwa sababu wanahitaji kuongoza kundi A japo wameshatinga robo fainali.

Wakati huo huo, klabu hiyo imesema tayari jumla ya Shilingi milioni 47 zimechangwa na mashabiki wa timu hiyo katika kampeni ya 'tunawajibika pamoja' kwa ajili ya kulipia fainali ya dola 40,000 walizotozwa na CAF.

"Pesa zilizopatikana mpaka sasa ni Shilingi milioni 47, 141, 024, na iliyobaki ni Sh. milioni 52, 858, 976," alisema Ahmed.

Ahmed alisema iwapo haitotimia klabu itaongezea kilichobaki na kama kiasi kitazidi basi kitatumika kwa matumizi mengine ya timu.