Ligi Kuu yaondosha makocha 13

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:08 AM Feb 10 2025
Patrick Aussems
Picha: Mtandao
Patrick Aussems

WAKATI mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara ukiwa umeanza, jumla ya makocha 13 wameziacha timu walizokuwa wakizifundisha kwa sababu mbalimbali, ikiwamo kutimuliwa kutokana na kufanya vibaya, au kuamua kuondoka wenyewe.

Hata hivyo, baadhi ya makocha wamerejea tena kwenye ligi na kuzifundisha timu zingine.

Rekodi zinaonesha kuwa makocha waliotimuliwa kwa timu kufanya vibaya ni David Ouma, raia wa Kenya, aliyekuwa akiinoa Coastal Union, Youssouph Dabo, Msenegal aliyekuwa Kocha Mkuu wa Azam FC, Mwinyi Zahera aliyekuwa akikinoa kikosi cha Namungo, , Mbelgiji aliyekuwa anaikochi, Singida Black Stars, Paul Nkata, Mganda aliyekuwa kocha wa Kagera Sugar, Mkenya Francis Kimanzi, aliyekuwa kocha wa Kagera Sugar, Mbwana Makata, Mtanzania aliyekuwa anaifundisha Prisons, Mohamed Muya wa Fountain Gate, na Miguel Gamondi, kocha wa zamani wa Yanga.

Hawa wote walitimuliwa na viongozi wa klabu zao baada ya kuona hawafanyi kile ambacho walitarajia kukifanya kwenye mchezo wa Ligi Kuu, hivyo kuoneshwa njia ya kutokea.

Makocha watatu, Fikirini Elias wa KenGold, Abdulhamid Moalin na Sead Ramovic, kesi zao za kuondoka kwenye klabu ni tofauti kidogo.

Fikirini alijiuzulu mwenyewe baada ya kuona hajafanya kile ambacho alikuwa anatarajia kwenye malengo yake kama kocha, na kabla hata viongozi hawajafanya chochote kutokana na timu kufanya vibaya, aliondoka.

Moallin aliyekuwa Kocha Mkuu wa KMC, alichukuliwa na Yanga, kwenda kuwa Mkurugenzi wa Ufundi, chini ya Sead Ramovic, baadaye akawa mmoja wa wasaidizi wake, na ameendelea na nyadhifa hizo chini ya kocha wa sasa, Miloud Hamdi.

Kocha Ramovic, ameondoka mwenyewe Yanga kwa makubaliano ya pande mbili, baada ya kupata dili nono kutoka Klabu ya CR Belouizdad ya Algeria.