KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani, Adam Mfilinge amezindua mashindano ya Judith Cup katika Kata ya Mbwawa yanayolenga kuhamasisha wananchi kujiandikisha katika daftari la mpiga kura.
Akizindua mashindano hayo ambayo yatahusisha mpira wa miguu , rede na michezo mingine Mfilinge amesema michezo ni kiunganishi ambacho kinaongeza mahusiano kwa Jamii.
"Nimeridhika na hiki kilichofanywa na Diwani Judith nimpongeze kwa hatua hii na biwaombe wananchi mnapopata kiongozi anayejua wananchi wanataka nini muungeni mkono kwa ajili ya maendeleo," amesema.
Amesisitiza wananchi kushiriki kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura pamoja na kupiga kura kuchagua viongozi makini ambao wataendelea kuungana na Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo.
Muandaaji wa Mashindano hayo Judith Muluge amesema mashindano hayo ni ya kutangaza kazi zilizofanywa na Serikali iliyopo madarakani sambamba na kuhamasisha wananchi kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Judith pia amesema mashindano hayo yatasaidia wananchi kupata muda wa kukutana kujadiliana mambo mbalimbali na vijana ambao hawana kazi kupata muda wa kufuatilia michezo ambayo inaambatana na ujumbe wa uchaguzi.
Zulfa Omari ni mmoja wa washiriki wa michezo hiyo upande wa rede ambaye amemshukuru Diwani kwa kuandaa mashindano hayo huku akiahidi kwenda kushiriki uhamasishaji wa wananchi kujiandikisha kwenye daftari kudumu la mpiga kura na kupiga kura.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED