BENCHI la ufundi la timu ya Kagera Sugar limesema litafanya usajili wa kishindo kwa ajili ya kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza na Nipashe jana, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Fred Felix 'Minziro' alisema malengo yake ni kuwa na kikosi chenye ushindani msimu ujao ili aweze kushika nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi hiyo.
"Malengo yangu ni kuongeza wachezaji wenye uwezo mkubwa ili tuendeleze ushindani wetu katika msimu ujao ambao naamini utakuwa bora zaidi, alisema Minziro.
Aidha, Minziro alisema msimu uliopita ulikuwa mgumu kwao na wenye ushindani kutokana na maandalizi yaliyofanywa na kila timu kuhakikisha haishuki daraja.
"Msimu uliopita nilibaini mapungufu ndani ya timu yangu ambayo nitayafanyia marekebisho ili yasijirudie katika msimu ujao," alisema Minziro.
Pia aliwashukuru mashabiki na wapenzi wa timu hiyo kutokana na ushirikiano waliowaonyesha katika kipindi chote cha ligi licha ya kutofanya vizuri kwenye baadhi ya michezo yao.
Timu hiyo imemaliza ligi ikiwa nafasi ya 13 ikiwa na pointi 32 na hivyo kusalia kwenye Ligi hiyo msimu ujao.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED