HATIMA ya Kocha Mkuu wa Pamba Jiji FC, Mbwana Makata na mshambuliaji wa timu hiyo, Jerry Tegete, kubakia ndani ya kikosi hicho iko mashakani, imeelezwa.
Pamba Jiji FC itashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao baada ya kumaliza katika nafasi ya pili kwenye Ligi ya Championship msimu huu.
Bingwa wa Ligi ya Championship, KenGold ya Mbeya pia imepanda daraja moja kwa moja huku timu nyingine mbili zitajulikana baada ya kumalizika kwa michezo ya mtoano.
Makata ameiwezesha Pamba Jiji FC kurejea katika Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya miaka 23 Pamba Jiji FC imerejea Ligi Kuu msimu huu na kunamfanya kocha Makata kuweka rekodi ya kuwa kocha pekee Tanzania ambaye amezipandisha daraja timu nne ndani ya misimu saba.
Kocha huyo pia aliwahi kuipandisha Alliance FC msimu katika mwaka 2017/18, Polisi Tanzania 2018/19, Dodoma Jiji 2019/20 huku Jerry Tegete, akiwa mmoja wa nyota walioipandisha timu hiyo.
Akizungumza na Nipashe jana, Ofisa Habari wa Pamba Jiji, Martin Sawema, alisema Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo itakutana kati ya Juni mwishoni au mapema Julai ili kujadili na kuweka mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuelekea msimu ujao.
“Hatutaki kuwa katika historia ya kupanda na msimu unaofuata kushuka, tunahitaji kufanya maboresho makubwa ndani ya kikosi ikiwamo usajili mzuri na kuangalia uwezekano wa kubakia na Kocha Makata.
Aliongeza kikao hicho kinatarajia pia kupokea ripoti ya kocha kuhusu mapendekezo ya nyota watakaosajiliwa kwa ajili ya msimu mpya kwa sababu wanataka kumaliza katika nafasi nne za juu.
“Kama tunahitaji kumaliza katika nafasi nne za juu na kutoshuka daraja, lazima tuimarishe kikosi, na kawaida kwa timu zinazopanda daraja kucheza Ligi Kuu zinatakiwa kufanya usajili mkubwa kwa kupunguza baadhi ya wachezaji waliopandisha na kuleta wengine,” Sawema alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED