Pep Guardiola amesema Manchester City bado inaweza kuifikia Arsenal katika mbio za kuwania taji la Ligi Kuu England msimu huu, akiwaonya wapinzani wao kwamba, "mengi yanaweza kutokea katika michezo 13 iliyobaki," baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Liverpool juzi, kupunguza pengo la pointi hadi sita kileleni mwa msimamo.
Mabao mawili katika dakika sita za mwisho ya Man City kutoka kwa Bernardo Silva na Erling Haaland yalifuta bao la kwanza la Dominik Szoboszlai la dakika ya 74 na kuipa timu hiyo ya Guardiola pointi tatu.
Man City watacheza na Fulham Jumatano kwenye uwanja wa Etihad, wakati Arsenal watasafiri kwenda kucheza na Brentford, Alhamisi.
Guardiola anaamini kwamba, mbio za ubingwa huo zinamaanisha Man City bado ina nafasi ya kuipiku Arsenal ya kocha Mikel Arteta na kuibuka mabingwa.
"Tuko nyuma kwa pointi sita," alisema Guardiola akiwaambia waandishi wa habari baada ya mchezo huo.
"Sawa, ni pengo kubwa, lakini mambo mengi yanaweza kutokea, kwa hiyo ni lazima tupate pointi tatu kila mchezo uliopo mbele yetu.
"Nani anajua kama pointi sita zinatosha kwa Arsenal, kuna michezo 13 ambayo ni mingi na Kombe la FA linakuja, fainali ya Kombe la Carabao pia, Ligi ya Mabingwa Ulaya inarudi Machi na majeraha yanaweza kutokea.
"Kwahiyo michezo 13 kutokana na uzoefu wangu ni mingi sana, lakini jambo muhimu ni kuwa tupo kwenye mbio. Tunachoweza kufanya ni kuipumulia Arsenal, kujaribu kuona kama watateleza.”
CHANZO: ESPN
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED