HATIMAYE michuano ya Umoja Cup Rorya 2024, imetamatika mwishoni mwa wiki kwa Gonga FC kutawazwa mabingwa wapya baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 7-6 dhidi ya wanafainali wenzao na mabingwa watetezi, Wanamaji FC.
Katika mtanange huo mkali wa fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa Maji Sota, Rorya, timu hizo zilifika hatua ya mikwaju ya penalti baada ya dakika 90 za mchezo kutamatika kwa sare ya mabao 2-2.
Gonga FC ya Busurwa ilitinga fainali baada ya kuwatupa nje Kabwana FC kwenye mchezo wa nusu fainali wakati waliokuwa mabingwa watetezi na wenyeji wa michuano hiyo, Wanamaji fc wakiwaondosha mashindanoni Bubombi fc.
Katika mashindano hayo ya kila mwaka ya Umoja Cup Wilaya ya Rorya ambayo yalianza tangu mapema Agosti mwaka huu na kujumuisha timu 18 kwa mfumo wa makundi, yalishuhudiwa pia timu ya Kabwana FC ikiibuka mshindi wa tatu baada ya kuitoa Bubombi FC.
Kwa kutwaa ubingwa huo Gonga FC imeondoka na kitita cha shilingi 500,000, seti moja ya jezi na kombe, huku Wanamaji FC wakitia kibindoni Sh. 200,000 na seti moja ya jezi kwa kumaliza nafasi ya pili.
Kabwana FC nayo ilizawadiwa seti moja ya jezi na Sh.100,000, kwa kushika nafasi ya tatu huku wanyonge wao, Bubombi FC wakiondoka na jezi seti moja na Sh. 50,000 kwa kushika nafasi ya nne.
Aidha, Thomas John alitangazwa kuwa Golikipa Bora wa mashindano hayo na kuzawadiwa Sh. 30,000 huku Mfungaji Bora akiwa ni Riziki Abega wa Wanamaji FC naye akiondoka na kitita kama hicho wakati Mchezaji Bora, Victor Simon wa Kabwana FC yeye akizawadiwa Sh. 40,000.
Mchezaji Bora Chipukizi, Yohana Masha wa Young Boys yeye alizawadiwa Sh. 20,000 huku Kocha Bora, Ochieko Bora wa Gonga FC akipewa zawadi ya Sh. 50,000 wakati Nyakina FC ilitangazwa kuwa timu yenye nidhamu na kuzawadi Sh. 30,000.
Mbali na zawadi hizo pia timu zote zilizoshiriki michuano hiyo mwaka huu, kila moja ilizawadiwa mpira mmoja.
Katika hatua nyingine, mdhamini wa michuano hiyo kwa zaidi ya miaka 11, Peter Owino, alitunukiwa cheti kutoka Chama cha Soka Wilaya ya Rorya (ROFA), kwa kutambua mchango wake uliotukuka wa kuendeleza na kukuza soka wilayani humo.
"Tunatoa pongezi za dhati kwa waandaaji wa mashindano ya Umoja Cup, wamejitahidi sana kufanya mashindano kuwa na utofauti kila mwaka, hongereni sana, hongera sana kwa mdhamini wa Umoja Cup [Peter Owino], Mwenyezi Mungu akupe maisha marefu kwa ajili ya furaha ya Wanaumoja Cup," alisema Afisa Michezo wa Wilaya ya Rorya, Said Masanja.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED