KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amezitahadharisha timu za Ligi Kuu Tanzania Bara zitapata 'tabu' kuwazuia wachezaji wake kufunga mabao kwa kutumia mipira ya faulo kwa sababu tayari mafunzo anayowapatia yameshaanza kufanya kazi.
Gamondi amesema amegundua katika Ligi Kuu Tanzania Bara, mipira ya faulo inapatikana mingi, lakini imekuwa haitumiwi vizuri, hivyo ametengeneza mafunzo maalum kwa nyota wake ili waweze kupata mabao kwa njia hiyo.
Kocha huyo alisema hayo baada ya mechi dhidi ya Pamba Jiji iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam na timu yake kuondoka na ushindi wa mabao 4-0.
Beki wa kati, Ibrahim Hamad 'Bacca', kwa mara nyingine tena alifunga bao akiunganisha kwa kichwa mpira wa faulo iliyopigwa na Maxi Nzengeli.
Licha ya kuwa ni bao la pili kwa Bacca, pia ni la pili lililotokana na mpira wa faulo, kama ilivyotokea, Septemba 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya dhidi ya KenGold, alipopachika bao kwa kichwa, kutokana na faulo iliyopigwa na Stephane Aziz Ki na kuwa bao pekee katika mchezo huo.
"Kwa sasa tumejifunza jinsi ya kupata mabao kwa njia ya faulo, kila kitu tumekifanyia mazoezi, katika ligi ya Tanzania wachezaji wanafanya faulo nyingi sana, kama zinatumiwa vizuri, tunaweza kupata mabao mengi na ndivyo ninavyofanya sasa," alisema Gamondi.
Kocha huyo alifurahishwa pia na safu yake ya ulinzi kuwa imara kwa kucheza michezo nane bila kuruhusu nyavu zao kutikiswa.
"Ikumbukwe tuna rekodi safi ya kucheza michezo nane bila kuruhusu bao, mara ya mwisho ilikuwa ni kwenye fainali ya Kombe la FA dhidi ya Azam FC, hii ni kazi kubwa ya mabeki wangu, wakisaidiwa na wenzao," alisema kocha huyo raia wa Argentina.
Aliongeza alijua Pamba Jiji wangeingia na staili ya kupaki basi, hivyo akawaandaa wachezaji wake kucheza na timu ya aina hiyo.
Ushindi huo umewafanya Yanga kufikisha pointi 12, ikishika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED