Fadlu afurahishwa ukomavu wa wachezaji wake vijana

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:12 AM Oct 01 2024
Wachezaji wa Simba.
Picha:Simba
Wachezaji wa Simba.

KOCHA wa Simba, Fadlu Davids, ameeleza kufurahishwa na wachezaji wake wengi vijana kwenye kikosi chake ambao hawana uzoefu na michezo mikubwa kumudu kucheza michezo mitatu mikubwa ndani ya siku saba tu na kushinda yote.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya timu hiyo dhidi ya wenyeji, Dodoma Jiji FC, kwenye Uwanja wa Jamhuri mchezo uliomalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0, kocha huyo raia wa Afrika Kusini amesema si rahisi kuwa na kikosi kama chake cha wachezaji wengi vijana ambao hawajawahi kucheza michezo migumu na yenye presha mbele ya maelfu ya mashabiki lakini wakaweza kumudu na kushinda yote.

"Ushindi wa bao moja, pointi tatu, tumeshinda bila kuruhusu bao, hii ni nzuri sana, nadhani tulichofanya hapa ni mwendelezo mzuri, lakini narudia tena kuwa tunacheza michezo hii katika mazingira magumu, tumecheza mechi tatu ndani ya siku saba tu, tena michezo migumu yenye presha kubwa sana ndani na nje ya uwanja kwa mashabiki wetu, tuna wachezaji wengi vijana hawajazoea hili, lakini wameweza kupambana na kuweza kufanya kazi kwa usahihi mpaka kupata ushindi wa asilimia mia moja," alisema Fadlu.

Juzi ilikuwa ni Jumapili ya kwanza tangu Simba ilipocheza mchezo wake wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya, Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikipata ushindi wa mabao 3-1, siku nne baadaye ikacheza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC, Uwanja wa New Amaan Zanzibar, kabla ya siku tatu baadaye, Jumapili iliyopita kushinda bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji, ikiwa ni siku ya saba.

Alisema katika mchezo wa juzi wachezaji wake walionekana kupata uchovu na ilionekana dakika za mwisho wa mchezo.

"Wachezaji wamepata fatiki, na hili limeonekana dakika za mwishoni mwa mchezo, hatukuwa na shepu nzuri ya kuzuia, mechi tatu kwa wiki ukichanganya na safari ndefu za Libya, Zanzibar na Dodoma zimeonekana kuwaathiri wachezaji wangu, lakini nawapongeza sana kwa sababu wanapambana sana na kupata ushindi licha ya uchanga wao," alisema.

Alisema katika mchezo huo, wachezaji wake kama wangekuwa makini wangeweza kumaliza mechi mapema tu, kwani walipata nafasi nne kipindi cha kwanza.

"Tulianza vizuri tumepata nafasi nne za kufunga, kama tungeweka mpira ndani ya wavu tungekuwa tumemaliza mchezo mapema, tulianza mchezo huu na washambuliaji wawili, tukabadilisha kipindi cha pili, kila kipindi kilikuwa na malengo tofauti," alisema Fadlu.

Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji, Mecky Maxime, kwa kiasi kikubwa alilia na mwamuzi, Omari Mdoe, akidai hakupaswa kutoa mkwaju wa penalti iliyowapa ushindi Simba kupitia kwa Jean Charles Ahoua.

"Mechi ilikuwa nzuri hata watazamaji wameinjoi, lakini imeamuliwa na makosa ya kibinadamu, sijaona vizuri, lakini nadhani beki wangu kwanza alicheza mpira," alisema.

Ushindi wa Simba, unaifanya kufikisha pointi 12 katika michezo minne iliyocheza na kushinda yote, lakini ikiendelea kusalia nafasi ya tatu huku Dodoma Jiji ikiporomoka nafasi moja kutoka ya tisa hadi ya 10, ikibakia na pointi zake sita baada ya michezo sita.