Bara, Zanzibar kuongeza uzoefu katika michezo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:20 PM Feb 19 2025
Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais, Abdallah Hassan Mitawi
Picha: Mtandao
Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais, Abdallah Hassan Mitawi

SERIKALI imetoa wito kwa Vyama vya Michezo vya Tanzania Bara na Zanzibar, kushirikiana na kubadilishana uzoefu, ili kuendeleza mshikamano baina ya wananchi wa pande zote mbili na kudumisha Muungano.

Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais, Abdallah Hassan Mitawi, akifungua Kikao cha Maandalizi ya Ligi ya Muungano kuelekea Maadhimisho ya Miaka 61 ya Muungano kilichofanyika jijini Dar es Salaam Februari 18, 2025.

Lengo la kikao hicho ni kufuatilia na kuweka mkakati wa kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano mwaka 2024 kuhusu kurejeshwa kwa Ligi ya Muungano kwa lengo la kudumisha Muungano.

Akizungumza na wadau wa michezo kutoka vyama mbalimbali nchini, Naibu Katibu Mitawi, amesema Wizara zinazosimamia Michezo zina wajibu wa kuhahakima azma ya Mheshimiwa Rais inatimizwa.

“Ndugu zangu, tunatambua kwamba michezo ilikuwa ni kielelezo cha mshikamano kwa watu kukutana na kutumia nafasi hiyo kupenyeza agenda zingine, hususani wakati wa kudai Uhuru,“ ameeleza.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu Mitawi ameongeza kuwa Wizara zinazosimamia sekta ya michezo Tanzania Bara na Zanzibar zina wajibu wa kuhakikisha azma ya Mhe. Rais Dkt. Samia inatimizwa.

Hivyo, Naibu Waziri Mkuu ametumia wasaa huo kuwasihi washiriki wa kika hicho kujadili kwa uzito na kutoka na maazimio ya namna bora katika kutekeleza agizo hilo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Muungano Ofisi ya Makamu wa Rais Dk. Juma Mohamed Salum amesema lengo la kukutana wadau hao na Serikali ni kujadili na kufikia hatua nzuri kuyafanya mashindano ya Muungano kuwa endelevu.