Bacca apania kuitungua Simba

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:20 AM Oct 07 2024
BEKI wa Kati wa Yanga, Ibrahim Hamad 'Bacca',
Picha:Mtandao
BEKI wa Kati wa Yanga, Ibrahim Hamad 'Bacca',

BEKI wa Kati wa Yanga, Ibrahim Hamad 'Bacca', amesema katika mwendelezo wake wa kusaka kiatu cha dhahabu, anatamani pia kufunga bao katika mechi ijayo dhidi ya Simba, Oktoba 19, mwaka huu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, mchezaji huyo alisema kwa sasa anatamani kufunga bao kwenye kila mchezo ambao timu yake inacheza hasa kwenye Ligi Kuu ambako ameamua kuingia rasmi kwenye kinyang'anyiro cha kuwania ufungaji bora.

Bacca, aliwashangaza mashabiki wa soka baada ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya KenGold, Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, akisema kuwa ameingia rasmi kwenye kinyang'anyiro cha kuwania ufungaji bora msimu huu.

Ilikuwa ni baada ya kufunga bao pekee kwenye mchezo huo uliopigwa uwanjani hapo Septemba 26, mwaka huu, Yanga ikishinda bao 1-0.

Ilionekana kama ni kufurahisha baraza, lakini waliwashtua wengi alipopachika tena bao, Alhamisi iliyopita, Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, Yanga iliposhinda mabao 4-0, dhidi ya Pamba Jiji FC.

"Wale waliokuwa wanadhani mimi natania nadhani wameanza kuamini, kama nilivyoweka ahadi yangu, nadhani huu ni mwanzo tu, unajua baada ya kufunga bao moja kule Mbeya, akili yangu sasa nataka kufunga bao kila mchezo unaokuja, na utakaofuata unajua tunacheza na nani Oktoba 19, nataka pia kufunga bao," alisema beki huyo ambaye pia anaichezea timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

Mchezaji huyo ambaye kwa sasa yupo kambini na Stars, alisema angekuwa na mabao matatu kama si kukatazwa kwenda kupiga penalti katika mchezo dhidi ya Pamba Jiji.

"Unaona hata ile penalti ilipotokea nilitaka kupiga mimi mwenyewe kuendeleza nilichoahidi, saa hizi ningekuwa na mabao matatu, anayeongoza kwenye ufungaji mpaka sasa si ana mabao matano jamani? Sasa matatu si yangebaki mawili tu, tungekuwa tunafukuzana," alisema Bacca na kulalamika juu ya kukatazwa kupiga penalti na nahodha wake, Bakari Mwamnyeto.