TAMASHA lililosubiriwa kwa hamu kubwa, Bata la Desemba, lililofanyika kuanzia Desemba 6 hadi 8, mwaka huu, katika viwanja vya Leaders Club, limehitimishwa kwa mafanikio makubwa likiwa na sherehe za kusisimua za muziki, utamaduni na mshikamano wa jamii.
Kwa ujumla tamasha hilo lilihusisha maonesho ya wasanii wakubwa wa Afrika, wakiwamo Zuchu, Master KG, Chino Kidd, Linah Sanga, Johmakini, G Nako, na wengine wengi ambapo watazamaji walifurahia mchanganyiko wa muziki, michezo, ucheshi na matangazo mubashara ya michezo, ambayo yaliendelea kuweka hewa ya shangwe kwa siku zote tatu.
Mbali na burudani, tamasha hilo pia lilitoa fursa kwa wachuuzi wa ndani, likionesha utofauti wa vyakula vya Dar es Salaam na kuwapa wajasiriamali wa ndani nafasi ya kuwasiliana na maelfu ya wateja watarajiwa, hiyo ikiendana na lengo pana la kusaidia uchumi wa ndani na kuunda fursa za ukuaji.
Tukio hili, lililoandaliwa na Heineken Beverages International kwa ushirikiano na Mkoa wa Dar es Salaam, limekusanya zaidi ya watu 3,000 kwa siku tatu za burudani ya kiwango cha juu, vyakula vya asili, michezo mubashara, na onesho la wasanii la kuvutia.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, hakusita kuelekezea fahari yake kwa mafanikio ya tamasha hilo.
“Tamasha la Bata la Desemba halikuonesha tu nishati ya kipekee ya Dar es Salaam bali pia liliangazia jiji letu kama kitovu cha utamaduni, biashara, na ukuaji wa uchumi. Tukio hili limeonesha umaarufu wa Dar es Salaam kama kitovu cha utalii na utamaduni huku tukisherehekea mshikamano na furaha inayotutambulisha kama jamii,” alisema.
Obabiyi Fagade, Meneja wa Nchi (country manager) wa Heineken Beverages International nchini Tanzania, alisema: “Mafanikio ya Bata la Desemba ni kielelezo halisi cha maadili tunayoyasimamia – kuwaleta watu pamoja kusherehekea, kuleta furaha, na kuchangia ustawi wa kiuchumi wa jamii ya hapa.
"Tukio hili halikutoa tu jukwaa la burudani ya kiwango cha dunia bali pia liliwaunga mkono wafanyabiashara wa ndani na wajasiriamali, likichangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania.”
Alisema katika kipindi chote cha tamasha, walionesha dhamira yao ya kukuza mshikamano na kushirikiana na kwamba tukio hilo halikuwa tu nafasi kwa Watanzania na wageni wa kimataifa kuungana, bali pia lilionesha uwezo wa kanda hii kama kiungo muhimu katika mazingira ya kiuchumi ya Afrika Mashariki.
Tamasha hilo lilimalizika kwa onyesho la fataki kusherehekea miaka 63 ya uhuru wa Tanzania ambapo washiriki walionesha furaha yao na shukrani kwa mazingira mazuri na utekelezaji mzuri wa tukio hilo. Wengi walilitaja kama tukio kubwa na la kukumbukwa zaidi kwa mwaka huu, huku mchanganyiko wa burudani, utamaduni, na mshikamano ukiacha athari kubwa kwa wote walioshiriki.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED