Samia amlilia mtunzi kibao Tanzania Yetu, kuzikwa kesho

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:23 PM Feb 17 2026
 Samia amlilia mtunzi kibao Tanzania Yetu, kuzikwa kesho
Picha:Mtandao
Samia amlilia mtunzi kibao Tanzania Yetu, kuzikwa kesho

Rais Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha mwanamuziki mkongwe nchini, Steven Hiza, aliyeimba kibao maarufu kiitwacho ‘Tanzania Yetu Ndio Nchi ya Furaha’.

Hiza (81), alifariki dunia jijini, Tanga jana jioni na  atazikwa kesho.

Akiwasilisha salamu za pole, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema Rais Samia amemtaja marehemu, Hiza kuwa msanii mahiri na mzalendo aliyetumia kipaji chake kuelimisha, kuburudisha na kuhamasisha jamii.

Makonda amesema marehemu alitumia sanaa ya muziki kama chombo cha kuimarisha maadili, umoja na utambulisho wa Taifa.

Rais ametoa rai wa wanamuziki na wadau wa tasnia ya muziki nchini kudumisha na kuenzi mchango wake mkubwa katika kukuza na kuendeleza muziki wa Tanzania.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Muziki wa Rhumba Tanzania, Hassan Msumari, amesema Hiza alifariki akiwa nyumbani kwao Mtaa wa Mwanzange, baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa pumu kwa muda mrefu.

Msumari amesema mwanamuziki huyo atazikwa leo katika Makaburi ya Goseji jijini hapa.

“Taratibu za mazishi zinaendelea vyema, Chama cha Muziki wa Rhumba Nchini kinaunga na familia ya mwanamuziki huyu mkongwe katika msiba huo, tunatoa pole kwa familia na wanamuziki wote Tanzania,” Msumari amesema.

Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Muheza, Hebert Mntangi, ameiambia Mipashe Digital alimfahamu vizuri mwanamuziki huyo ambaye alitumia kipaji chake kueleimisha jamii.

Mwanamuziki huyo ndiye mtunzi wa wimbo wa 'Tanzania Yetu' ambao aliutunga na kuurekodi kwenye studio za Redio Tanzania Dar es Salaam mwaka 1966, akiwa na bendi ya Atomic Jazz, iliyokuwa na maskani yake Tanga.

Wimbo huo umekuwa ukipigwa katika hafla mbalimbali za kitaifa na ukilenga kuelezea umoja, mshikamano na upendo kwa Watanzania.

Mwaka juzi, Rais Samia alimzawadia marehemu kiasi cha Sh. milioni 50 pamoja na tuzo kutokana na mchango wake mkubwa katika tasnia ya muziki.