Fadlu azifanyia umafia, ASEC, Al Masry CAF

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:04 AM Feb 10 2025
ocha Mkuu wa Simba Fadlu Davids
Picha: Mtandao
ocha Mkuu wa Simba Fadlu Davids

WAKATI akiwa anaendelea kukiongoza kikosi chake na michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Kocha Mkuu wa Simba Fadlu Davids, ameanza kazi ya kuzifuatilia na kuzichunguza timu tatu za ASEC Mimosas ya Ivory Coast, Al Masry ya Misri na Stellenbosch FC ya Afrika Kusini, ambazo moja kati ya hizo watakutana nayo kwenye mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally, amebainisha hayo, akisema Fadlu hana muda wa kupoteza kwani ameanza kazi hiyo ili iwe rahisi kuwaelekeza wachezaji wake la kufanya pindi droo itakapochezeshwa Februari 20, mwaka huu.

Alisema kocha wao amekuwa akifanya kazi mbili kwa wakati mmoja, kuwaweka sawa wachezaji wake kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu, lakini pia kuzifuatilia timu hizo tatu kujua ubora na udhaifu wao.

"Ukitaka kujua kuwa msimu huu tuko makini na kila michuano ndiyo hapa sasa, tuko kwenye Ligi Kuu, lakini bado kocha pia amekuwa akizichunguza timu ambazo tutacheza nazo. Katika timu hizo tatu ni lazima moja tuchezea nayo, kwa hiyo kama akizifanyia kazi, ina maana ikija kuwekwa wazi ni ipi, basi wala hatopata tabu, atajua tu timu hiyo iko vipi, unachezaje, ubora wake uko wapi, udhaifu na  wachezaji wetu wafanye nini ili kuidhibiti," alisema Ahmed.

Wekundu wa Msimbazi walimaliza kileleni mwa msimamo wa Kundi A, Kombe la Shirikisho linaloandaliwa na Shirikisho la Afrika (CAF), wakijikusanyia pointi 13, wakifuatiwa na CS Constantine waliomaliza nafasi ya pili na alama 12 na zote zimetinga hatua ya robo fainali, huku Bravos do Maquis ya Angola na CS Sfaxien ya Tunisia zikitupwa nje.

Kuhusu kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Ahmed amesema hawana wasiwasi na hilo, akiwahakikisha wanachama na mashabiki wa timu hiyo kuwa zipo mechi ambazo watani wao wa jadi, Yanga watapoteza, ikiwamo ile ya Machi 8, mwaka huu, ambayo itazikutanisha timu hizo mbili.

"Hatuna presha juu ya kurejea kwenye nafasi yetu, bado kadhaa turejee kileleni, ninaimani tutafanya vizuri na wachezaji kuwapa furaha mashabiki na Wanasimba," alisema.

Pamoja na kwamba mara nyingi mechi za watani huwa hazitabiriki, Ahmed amesema hawatakubali kupoteza kwa mara nyingine mbele ya mahasimu wao hao.

Simba ilipoteza nafasi yake ya kuongoza Ligi Kuu Tanzania Bara ilipolazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Fountain Gate, mechi iliyochezwa, Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati mkoani Manyara, ambapo bao la kusawazisha la wenyeji wao lilifungwa na Ladack Chasambi, aliyejifunga mwenyewe baada ya kumrudishia kipa Moussa Camara pasi ndefu ya kasi.

Kabla ya hapo, ilikuwa ikingoza kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya Yanga, lakini kwa sasa nayo imeshushwa hadi nafasi ya pili, ikiwa na pointi 44, ikiachwa kwa alama moja na wapinzani wao hao.