Hatua zichukuliwe kudhibiti ajali mwishoni mwa mwaka

Nipashe
Published at 10:42 AM Oct 24 2024
Hatua zichukuliwe kudhibiti   ajali mwishoni mwa mwaka
Picha: Maktaba
Hatua zichukuliwe kudhibiti ajali mwishoni mwa mwaka

ZIKIWA zimebaki siku 69 kumaliza mwaka wa 2024, tayari ajali za barabarani zimeibuka na kugharimu maisha ya watu. Majira kama haya, ajali kama hizo zimekuwa zikipamba moto hivyo kusababisha watu kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa na kupata ulemavu wa kudumu.

Ndani ya wiki moja tangu Jumamosi iliyopita, kumetokea ajali tatu za barabarani ambazo zimesababisha watu 27 kufariki dunia na wengine 78 kujeruhiwa. Ajali hizo zimetokea katika mikoa ya Kilimanjaro na Mwanza. 

Katika ajali iliyotokea Oktoba 19, mwaka huu, katika eneo la Kikavu, Hai mkoani Kilimanjaro, iliyohusisha magari matatu yakiwamo Toyota Coaster na malori mawili, kwa mfano, watu 14 walifariki dunia ama papo hapo au hospitalini wakati wakipatiwa matibabu na wengine 12 kujeruhiwa. 

Wakati taifa likitafakari tukio hilo, juzi ziliibuka habari zingine za vifo vya watu 13 na wengine 59 kujeruhiwa katika ajali mbili tofauti. Ajali ya kwanza ni ile iliyohusisha mabasi ya Nyehunge na Asante Rabi kugongana katika eneo la Ukiliguru, Misunwi mkoani Mwanza na kusababisha vifo vya watu wanane na kujeruhi wengine 39. 

Ajali ya pili ilitokea usiku wa kuamkia juzi katika eneo la Kirinjiko, wilayani Same, Kilimanjaro ambayo ilisababisha vifo wa waimbaji watano wa Kwaya ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP) Usharika wa Wazo, Dar es Salaam. Katika ajali hiyo pia waimbaji wengine 20 waliokuwamo katika Toyota Coaster walijeruhiwa. 

Kwa takwimu hizo, ajali hizo zimesababisha kutoweka kwa nguvu kazi ya taifa na watu waliokuwa wakihitajika sana katika familia na jamii kwa ujumla, hivyo ni pigo kubwa. Sababu zinazoelezwa kuwa chanzo cha ajali hizo ni zile zile zikiwamo madereva kutokuwa makini  kwa kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari na kusinzia kwa uchovu. 

Wahenga wanasema dalili ya mvua ni mawingu. Kwa msemo huo ni kwamba hizo ni kama salamu za mwisho wa mwaka kwamba mambo yameshaanza. Hali hiyo pia inatoa ujumbe kwa vyombo vilivyopewa jukumu la kusimamia usalama barabarani kwamba vikae chonjo mambo yameshaanza. 

Kama ilivyo ada, ifikapo mwishoni mwa mwaka, ajali kama hizo zimekuwa zikiripotiwa mara kwa mara ambazo zimekuwa zikisababisha watu kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa, hivyo kubaki na ulemavu wa kudumu. 

Kuwapo kwa ajali hizo na sababu zikielezwa kuwa ni mwendokasi, madereva kutokuchukua tahadhari wakati wa kuyapita magari mengine na uzembe au usingizi wa madereva kusinzia kwa sababu ya uchovu. 

Ni wakati mwafaka sasa kwa vyombo vya usimamizi wa usafiri na usafirishaji kama vile Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) kuchukua hatua zinazostahili ili kudhibiti na kupunguza matukio hayo.

Bila shaka, kuwapo kwa matukio hayo yanayojirudia mara kwa mara huku nguvu kazi ya taifa ikiathirika, kuna tatizo mahali ambalo linapaswa kupatiwa ufumbuzi. Kama ni sheria kutokuwa kali, basi ni wakati mwafaka kuzifanyia mabadiliko ikiwamo faini na adhabu zinazotolewa kuongezwa makali zaidi. 

Aidha, ni vyema vitengo vya ukaguzi wa mabasi ya abiria vikaimarishwa ili kusiwapo mwanya wa kuruhusu magari mabovu au yenye kasoro kuingia barabarani, hivyo kusababisha ajali na kugharimu maisha ya watu. 

Ni matumaini kwamba iwapo kutakuwa na usimamizi wa kutosha ikiwamo kuchukua hatua zinazostahili, Tanzania bila ajali inawezekana.