Zuma; babu mwenye miaka ‘81’ anayejihisi ana nguvu kuongoza

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:03 AM Apr 17 2024
Mzee Jacob Zuma, katika picha tofauti.
Picha: Maktaba
Mzee Jacob Zuma, katika picha tofauti.

NCHI ya Afrika Kusini, ambayo inaongozwa na chama tawala cha African National Congress (ANC), inatarajia kufanya uchaguzi mkuu Mei 29 mwaka huu.

Katika uchaguzi huo, mwanasiasa mkongwe ambaye pia amewahi kuwa Rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma kabla hajafukuzwa ANC, anatarajia kuwania urais kupitia chama chake kipya cha uMkhonto we Sizwe (MK).
 
 Zuma anaingia katika kinyang'anyiro baada ya Mahakama ya Uchaguzi nchini humo, kubatilisha uamuzi uliomwekea kikwazo kiongozi huyo kugombea urais katika uchaguzi huo.
 
 Awali, Tume Huru ya Uchaguzi nchini humo ilimtengua Zuma kutogombea nafasi hiyo kwa mara nyingine kutokana na rekodi za uhalifu alizokuwa nazo.
 
 Hata hivyo, baada ya mahakama kumpa kumruhusu, ni wazi sasa atachuana na Rais wa sasa Cyril Ramaphosa aliyetangaza siku ya Jumatano kuwa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo utafanyika Mei 29. 

Tume ya Uchaguzi, nayo imetamka itakata rufani kusimamia uamuzi wake Zuma, asigombee.

Chama ambacho kitashinda wingi wa viti katika bunge lenye viti 400, vitamchagua Rais. Ramaphosa anagombea muhula wa pili wa miaka mitano ya mwisho.
 
 Zuma mwenye umri wa miaka 81, atagombea nafasi hiyo kupitia chama chake kipya alichokisajili baada ya kujitoa uanachama wa chama chake cha zamani cha ANC ili kuendelea na harakati za kisiasa.
 
    KUONDOLEWA ANC
 
 Mwaka 2018, Zuma alijiuzulu nafasi ya urais baada ya shinikizo kutoka katika chama chake cha zamani cha ANC, ingawa alipimga sana uamuzi wa kumshikiniza kujiuzulu.
 
 Kiongozi huyo aliyeingia madarakani tangu mwaka 2009, alikuwa akikumbwa na shutuma nyingi za ufisadi. Pamoja na kujiuzulu ameendelea kuandamwa na wabaya wake kisiasa.
 
 Katika kesi yake kuna shahidi mmoja aliyewahi kumshtumu kuwa alikuwa akipokea rushwa kila mwezi kutoka kampuni ya usalama, katika kashfa nyingine, ikaelezwa kuwa alilipwa fedha taslimu, zilizowekwa kwenye mkoba na kupelekwa na mtu maalumu.
 
 Hiyo inatokana na kwamba, bado hawajaridhika na hukumu iliompa ruhusa ya kuwani urais, na huenda wanamhofia, kwani wachambuzi wa siasa za kimataifa wanasema chama chake kipya hakitabiriki katika kinyang'anyiro hicho, kwamba kinaweza kupenya.
 
 Hayo ni kwa sababu wanaeleza kuwa kina ushawishi mkubwa katika jimbo analotoka Zuma la KwaZulu-Natal, huku akiahidi kubadilisha Afrika Kusini na inasemekana kuwa chama tawala kiko katika hatari ya kupata chini ya asilimia 50 ya kura kwa mara ya kwanza tangu kilipoingia madarakani mwishoni mwa enzi ya utawala wa ubaguzi.
 
 Zuma mwenyewe amekuwa akipiga kampeni kwa niaba ya chama cha upinzani cha uMkonto we Sizwe (MK) kwa lengo kufufua tena hadhi yake, akidai kuwa wanachama wa ANC ni wasaliti.
 
 Aidha, mwanasiasa machachari nchini humo, Julius Malema na chama chake cha Economic Freedom Fighters (EFF) naye ni miongoni mwa walioshiriki katika harakati za kuhakikisha Zuma anatoka madarakani.
 
   JACOB ZUMA NI NANI?
 Historia inaonyesha kuwa yeye ni miongoni mwa wapigania uhuru wa Afrika Kusini na kwamba, akiwa na miaka 17, alijiunga na ANC na kuwa mwanachama hodari katika tawi lake la jeshini Umkhonto We Sizwe, 1962.
 
 Katika harakati hizo za kutafuta uhuru wa nchi hiyo, alihukumiwa kwa kula njama za kutaka kupindua serikali ya kibaguzi na kufungwa miaka 10 katika gereza la watu hatari zaidi katika kisiwa cha Robben pamoja na Nelson Mandela.
 
 Inaelezwa kuwa Zuma alikuwa akichochea morali ya wapigania uhuru kwa nyimbo na tungo za kizalendo na wengi wanaamini kuwa hicho ndicho kilimfanya kuwa maarufu miongo ni mwa wananchi wa vijijini kabla ya kuupata urais.
 
 Yeye ni miongoni mwa walioishi Morogoro Tanzania wakati wa kupigania uhuru wa nchi yao, baadaye alikuja kuwa Rais wa Afrika Kusini kabla ya kujiuzulu kwa kashfa.
 
 Hata hivyo, akiwa madarakani, mwanasiasa machachari nchini, Julius Malema na chama chake cha Economic Freedom Fighters (EFF) walifanya mara kadhaa majaribio kutaka kumtoa madarakani. 
 
 Mwisho wake mwaka 2018 Zuma aliondolewa madarakani, hata hivyo, katika hatua hizo za kumzima kisiasa, mwanasiasa huyo mkongwe akaibuka na chama chake kipya.
 
 Zuma ndiye aliyemrithi Thabo Mbeki ambaye naye alijiuzulu nafasi hiyo  mwaka 2008 na kuamua kujiweka pembeni. Lakini kwa Zuma sivyo, bado anaendeleza harakati za kisiasa kupitia chama chake.
 
 Mbeki aliiongoza Afrika Kusini tangu Nelson Mandela alipostaafu  mwaka 1999 na alikuwa akitarajiwa kung'atuka mwaka 2009 lakini akajiuzulu na kumpisha Zuma ambaye naye yalimkuta mwaka 2018.
 
 Hata hivyo, pamoja na kumwekea zengwe akajiuzulu, Zuma bado hajapoa, wachambuzi wa siasa za kimataifa wanasema, huenda akafanya maajabu katika uchaguzi ujao, licha ya umri kumtupa mkono.