HUKO nyuma kihistoria, wakazi wa kijiji cha Rwakaremera katika kata ya Kasulo wilayani Ngara mkoani Kagera, hali ilikuwa mbaya kufikia huduma ya afya.
Walikuwa nyuma na maisha ya kutumia Sera ya Afya ya Mwaka 2017, inayotaka kila kijiji kuwa na zahanati, kata kuwa na kituo cha afya, wilaya hospitali, pia mkoa kuwa na hospitali ya rufani.
Ni madhila yaliyowafikisha kuchangishana kila kaya Sh.20,000 na zikapatikana Sh. milioni 30, wakaanzisha ujenzi mwaka huo 2021 hadi kufikia boma na baadaye serikali ikatoa Sh. milioni 50 za ukamilishaji, kazi iliyotimia mwaka 2022 na kuanza kutolewa huduma za tiba.
Hata hivyo, kukaibuka changamoto nyingine ya kukosekana nishati umeme katika zahanati, sasa ikidumu miaka mitatu hata ikabaki kwa dharura ya mgonjwa usiku pekee.
Inapotokea, watendaji wanalazimika kutumia tochi ya mlinzi au simu ya mtoa huduma wa zamu usiku, ndio chanzo cha mwanga, jambo linalowanyima amani na sasa wanaiangukia serikali kuharakisha utatuzi wake wa umeme unaojitosheleza.
Hiyo inachukua nafasi sasa, huku kukitajwa kitakwimu ujenzi huo umesaidia kuongeza idadi ya wagonjwa wa nje (OPD) wanaofika kupata huduma wakiwa 42,252,741 mwaka jana, kwa mujibu wa ripoti za ziara za kiafya; kutoka 41,347,690 mwaka 2022. Ni ongezeko la wagonjwa 905,501.
Katika idadi hiyo, waliopata huduma ngazi ya zahanati walikuwa asilimia 33, wenye rufani vituo vya afya asilimia 18, hospitali za halmashauri asilimia 23, asilimia tisa, Kanda na Taifa asilimia 17.
John Nkwale, mlinzi wa zahanati hiyo anaeleza namna amekuwa akiitumia tochi yake usiku kuwa msaada kwa wagonjwa wa dharura usiku na kikwazo hicho kimewafanya baadhi ya wagonjwa kwenda vituo jirani.
“Zahanati haina umeme, isipotumika simu za watoa huduma basi jua tochi yangu itatumika kama mwanga…” anaongeza Nkwale.
MGANGA MFAWIDHI
Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo, John Samwel, anakiri hali hiyo, hata wanatoa huduma mchana pekee na usiku hakuna mjamzito walishampokea, zaidi ya wagonjwa wa kawaida.
Anasema, kila katika kliniki za wajawazito, wamekuwa wakiwasisitiza kuhifadhi fedha za dharura kila wanapokaribia kujifungua, waweze kusafiri mpaka hospitali jirani za Lukole, Kasulo na Nyamiaga kupata huduma ya uzazi.
Dk. Samwel anasema kwa mwezi mmoja, wajawazito wanaofika kupata huduma kwake ni kati ya 30 mpaka 50 na kuna mwezi idadi ilishafika 80, huku malengo waliyopewa wagonjwa wasishuke chini ya 15, hivyo kituo kinahitajka kuongezwa ukubwa hasa upande wa kliniki.
Anafafanua kuwa, kituo kina mabenchi sita, mawili kati yake yanatumiwa na wagonjwa wa nje na manne wanatumia wajawazito wanaofika kliniki na kuna wakati wanalazimika kukaa chini ya miti inayozunguka zahanati.
Dk. Samweli anasema, zahanati ina umeme wa jua (Sola), lakini unatumika kuhifadhi dawa na vitu kwenye friji tu na hautakiwi kutumika kwenye vyumba vingine, ndio sababu ya kukosa umeme.
Anasema awali alishirikisha serikali ya kijiji kuangalia namna ya kufikisha umeme na zilitakiwa nguzo mbili kwa Sh.600,000, kutoka kwenye chanzo kikuu, lakini ulipofanyika upembuzi yakinifu awamu nyingine, zilihitajika nguzo nne kwa Sh. milioni nne, zilikwishalipwa TANESCO kuleta umeme.
Dk. Samwel anafafanua kuwa zahanati ilishindwa kufikisha umeme kwa sababu mapato yao yameelekezwa kwenye matumizi mengine kama kununua dawa, hivyo wakachukua hatua kuomba msaada wilayani kupitia Ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya, sasa muda wowote umeme utapatikana.
UONGOZI KIJIJI
Mwenyekiti wa Kijiji cha Rwakaremera, Jonathan Zofilo, anasema kukosekana nishati hiyo imebaki kikwazo kwa watoa huduma na wagonjwa zahanati husika, akihimiza kutafutwa suluhisho haraka kuepuka anachokiita ‘watajifungulia gizani.’
Diwani wa Kata ya Kasulo Yusufu Katura, anasema awali kila mwezi wajawazito watano mpaka nane walijifungulia njiani wakienda Kituo cha Afya Lukole, umbali wa kilomita 14 kutoka kijijini hapo au Hospitali ya Nyamiaga kilomita 45. Hata hivyo, jema hakuna vifo vilivyojitokeza.
WANANCHI KASULO
Christina Julius, mkazi wa kitongoji cha Njiapanda, anasema, lengo la kujenga na kusogeza huduma karibu ilikuwa kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu na kukabili dharura za kitabibu, kwani walishayona madhara, hasa kwa wajawazito na watoto wachanga.
“Mwaka 2018 ndugu yangu aliwahi kujifungulia njiani akielekea kituo cha afya Lukole kujifungua, nilishuhudia adha alizozipata na ‘Mungu saidia’ alijifungua salama, ila tulimsaidia.
“Tulikuwa naye na watu waliokuwa wakipita njia! Nilipoambiwa suala la kuchangia ujenzi wa zahanati, sikusita kwa sababu umuhimu wake naufahamu,” anasema Christina.
Aniceth Andrew, anayeishi kitongoji cha Nguvukazi, anasema siku za kliniki zao wamekuwa wakikumbushwa kujiandaa kwa fedha za usafiri kwenda hospitali kupata huduma, kwani inapotokea anapata uchungu usiku, hawezi kupata huduma zahanati kwa sababu ya kukosekana umeme.
“Wajawazito wanahudhuria tu kliniki ili kujua maendeleo ya watoto wao tumboni, inapofika muda wa kujifungua tunalazimika kuwasafirisha mpaka Hospitali ya Nyamiaga kilometa 35 mpaka 40 au Kituo cha Afya Lukole, kilometa 14, wapo tunaokutana nao wamejifungua njiani,” anasema Andrew.
Anasema, ni kawaida kliniki zote za wajawazito wanasisitizwa kuhifadhi fedha za dharura, anapokaribia kujifungua, asafiri mpaka hospitali jirani kama ya Lukole.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED