KADRI uzoefu wa mama aliyekwisha jifungua na hasa ambao kipindi cha ujauzito wamepitia changamoto kama vile uzazi pingamizi wakati wa kujifungua, huchangia kuwa na hofu ya uzazi ufuatao na hata kuathiri afya ya akili.
Mratibu wa Afya Akili na Utengamao wa Halmashauri ya Arusha, Dk. Paschal Kang’iria, anasema hali hiyo ndio ugonjwa wa akili unaoitwa sonona wakati wa ujauzito, huku hali hiyo ikimwathiri mama aliyetoka kujifungua.
“Mabadiliko ya homoni kipindi cha ujauzito na baada ya kujifungua ni jambo la kawaida, ingawa ugonjwa usipotibiwa, huwateteresha baadhi ya kinamama,” anasema.
Dk. Kang’iria ametamka hayo mwishoni mwa wiki, wakati akitoa elimu kuhusu afya ya akili kipindi cha ujauzito na baada ya kujifungua. Kwamba hali ya tashwishi kwa mjamzito au aliyetoka kujifungua, husababisha utengamao duni kiakili.
“Afya ya akili naifananisha na barabara, asubuhi na jioni foleni ni kubwa, ndivyo ubongo unafanya kazi kwa vipindi tofauti,” anaelimisha Dk. Kang’iriaAna ufafanuzi zaidi kwamba: “Barabara yenye msongamano barabarani, piga picha kichwani mwako pia unakuwa na msongamano wa mawazo. Afya ya akili huamua namna tunavyohisi, tabia zetu ni kama mwili ukiyumba ukachoka na akili inachoka pia.
“Ni afya ambayo inategemea namna unavyojifungamanisha na jamii. Mwingine timu yake ya mpira ikifungwa kesho akija ofisini anajisikia vibaya, anataniwa, anakuwa mnyonge hapa afya yake akili haiko sawa.
“Fikiria mama mwenye uzoefu wa kujifungua watoto wa jinsi moja, anawaza sijui nitapata tena mtoto wa sita wa kike? Mume wangu atanielewaje?
“Au mama kila anapojifungua anapitia uzazi pingamizi, anawaza safari hii nitajifungua kawaida au kwa upasuaji? Hofu, wasiwasi, maumivu ya ‘labour’ (chumba cha kujifungua), hasa kwa ambao ni uzazi wa kwanza. Hali hizo zikidumu, afya ya akili inayumba.”
Anasema changamoto iliyoko hivi sasa, hata kukuza magonjwa ya akili kama vile sonona, msongo wa mawazo kwa kundi hilo, ni kukosa uhusiano wa karibu na familia, wenza au jamii.
“Wanandoa au wenye uhusiano, hata ‘single mother’ (mama asiyeolewa), ana ujauzito, baba hamwoni, hata walio kwenye ndoa baadhi ndoa haijatulia mawazo muda wote, mama huyu huathiri afya ya akili,” anaongeza Dk. Kang’iria.MSAIKOLOJIA TIBA
Msaikolojia Tiba kutoka Hospitali ya Saifee, Dar es Salaam, Sifa Hyera, anasema athari za sonona kipindi cha ujamzito na baada ya mama kujifungua, zisipotibiwa mapema, humwathiri mtoto aliyeko tumboni na akishazaliwa humsababisha kuwa na uhusiano duni kijamii.
Katika tamko lake mwishoni mwa wiki kwenye mjadala wa elimu ya afya ya akili kwa mama, Sifa anaungana na mtaalamu mwenzake, akisisitiza umuhimu wake, kabla na baada ya kujifungua; kupunguza madhara ya sonona.
Ni mjadala ulioandaliwa na Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe (MNH), Sifa, akiitambulisha sonona kwa mjamzito, inavunja anachokitaja kitaalamu ‘bond’ (nguzo) ya mapenzi kati ya mama na mtoto.
“‘Bond’ ni muunganiko wa kihisia na kimwili, ambao huanza wakati wa ujauzito na kuendelea katika maisha ya mtoto.
“Mabadiliko ya homoni ni kawaida kwa mjamzito, lakini ikisababisha sonona humwathiri mtoto, ila hutibiwa kisaikolojia au dawa,” anasema.
Mtaalamu huyo anasema magonjwa ya akili yapo aina nyingi, ikiwamo sonona, inayuhusiana na hisia na hutafsiriwa kwa dalili kama endelevu ya huzuni, kupoteza hamu, pia hasira.
“Sonona huonekana kwa dalili tofauti kwa kipindi cha wiki mbili, kwa mgonjwa kukata tamaa, kukosa usingizi au kulala kupitiliza, kushtuka usingizini, kula zaidi au kula kidogo,” anaeleza.
Pia, anataja vyanzo vya sonona viko vingi, ikiwamo katika vinasaba ndani ya ukoo au familia kurithishana.
Kadhalika, msaikolojia tiba huyo, anasema hali alizokutana nazo mara kadhaa kwenye taaluma yake, nyingi amebaini wanaougua, chanzo ni kutokana na ugomvi kati ya mtu au jamii inayomzunguka kwa muda mrefu.
“Sonona inatibika, mojawapo ni kwa kutumia dawa na nyingine ni ya ‘saikotherapi’ (tiba saikolojia) kutoka kwa wasaikolojia tiba.
“Sonona kwa mjamzito, dalili hufanana na sonona za kawaida, mtu kupoteza ‘interest’ (mapenzi)... kuwa na huzuni kupitiliza, hamu ya kula haipo, kapungua au kuongezeka uzito.
“Au mama anakuwa na hofu, hasa akihofia muda wa kujifungua atakapokuwa ‘labour’. Mtu akiwa mjamzito kuna kuwa na homoni huwa zinaongezeka na kusababisha mabadiliko ya kihisia.
“Kwa ambaye hajaolewa au uhusiano haueleweki, anaweza kujikuta kwenye sonona ya kipindi cha ujauzito,” anasema mtaalamu Hyera.
Pia, anaeleza kuwapo athari kwa mtoto, iwapo mjamzito atakuwa na sonona, anakuwa hatarini kuzaliwa njiti, au kutokuwa sahihi na akawa anabadili hatua za ukuaji taratibu sana.
“Homoni ya mapenzi ikiachiliwa inaweka ‘bond’ ya mapenzi kati ya mama na mtoto aliyeko tumboni na mama. Ingawa mama akiwa mjamzito si kwa kupenda kwake, bali kile alichokuwa anakiwaza, akaingia katika sonona, muunganiko wao utapotea.
“Matokeo ya sonona kwa mjamzito ni mtoto atakayezaliwa kuwa na hasira, kukosa upendo, kuhusiana na watu akikua. Mtoto huyo pia anaweza akaja kupata magonjwa ya akili hapo baadaye akikua.
“Si watoto wote wanaozaliwa na kinamama waliopitia sonona wakawa na matatizo hayo, lakini inaweza kuchangia matokeo hayo kwa mtoto kwa kiwango kikubwa.
“Asilimia 60 ya wajawazito wanapitia sonona duniani, lakini inatibika, iwapo utafika kupata matibabu mapema, ili kupunguza athari hasi kwa mtoto kabla ya kuzaliwa,” anasema.
BAADA KUJIFUNGUA
Sifa anasema kwamba, mmoja kati ya kinamama saba, huweza kuwa na sonona baada ya kujifungua na dalili kuwa ni zilezile, kama; hasira, kujiona hawafai hata kuwaza kujidhuru au kumdhuru mtoto uliyemzaa.
“Mama akishajifungua hubadili ratiba, kulala, kuamka, hivyo kama hakujiandaa, anaweza kupata sonona. Nakumbuka Muhimbili (MNH), kulikuwa na ‘kesi’ mama aliyejifungua akapata sonona na kuanza kumdhuru mtoto.
“Tatizo kuu ni changamoto kwa mtoto kukosa kujenga muunganiko kwa jamii, hana uhusiano wa kijamii, anachelewa kukua na atasumbuliwa na vingi,” anahitimisha.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED