‘Wasioona wanafanya makubwa njooni VETA Dar mjithibitishie’

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 05:48 PM Jul 16 2024
 



Raphael Mwambalaswa.
PICHA: CHRISTINA MWAKANGALE
Raphael Mwambalaswa.

WATU wanaoishi na ulemavu wanadhihirisha kuwa wana fursa na uwezo wa kufanya mambo ya kujivunia, anasema Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Raphael Mwambalaswa.

Ni miongoni mwa wanafunzi wa Chuo cha VETA Dar es Salaam, anayekamilisha shahada ya uzamivu (PhD), kwenye kutengeneza madirisha ya alminiam.

Kwa juhudi hizo, anapingana na dhana kuwa wenye ulemavu mchango wao ni duni katika uzalishaji na kukuza uchumi, akisema wakipewa nafasi wanafanya makubwa.

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), inawatumia wenye ulemavu, wakijifunza teknolojia tofauti kwenye vyuo vyake.

Kuanzia mwaka 2022/2023 wanafunzi wenye ulemavu waliodahiliwa ni 602 huku waliotoka kwenye mazingira magumu ni 1,712 ambao wanapata mafunzo kama useremala, ujenzi, ushonaji na ufundi simu janja.

Mwambalaswa, asiyeona, anazungumza na Nipashe katika Banda la VETA kwenye Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam-Saba Saba, akisema, anafanya utafiti, kupata majibu ya kukabiliana na changamoto kwa wenye ulemavu mfano wasioona.

“Takwimu za ujifunzaji zinabainisha uwezo wa kuelewa kwa asilimia 80 unategemea macho, nikajiuliza kwa namna gani kundi la wasiiona ambao ni watoto watafanya nini ili kufikia asilimia 80 ambayo wao wanaikosa kwa sababu hawaoni ?”

"Nimesoma machapisho na utafiti unaonyesha asilimia 80 ya kujifunza hutegemea macho. Nikaamua kujikita katika eneo hili kwa kuwa na mimi nina ulemavu wa macho.

"Nikajiuliza changamoto ni zipi kwa watoto wasioona, ambao hushindwa kuifikia asilimia hiyo, wakiwa wanajifunza mfano darasani.”

Anasema anafanya ufundi mwenyewe wa kutengeneza madirisha ya aliminium chuoni VETA, kukamilisha PhD. 

Mwalimu wa VETA, Kintu Kiranga, anasema chuo hicho hupokea makundi tofauti ya wanaohitaji kujifunza, ikiwamo watu wenye ulemavu wa aina tofauti.

Anasema Mwambalaswa alifika chuoni hapo, ili kukamilisha PhD kwa kufanya ufundi, kwa kutengeneza madirisha ya alminiam.

“Anaweka vifaa vyake stoo na anajua kipi kinakaa wapi. Anafanya mwenyewe kila kitu kama vile kukata vipande vya madirisha na kuviunda, ni mara chache tutampa msaada.

“Wanafunzi wa aina hii wanatumia uwezo mkubwa wa mguso yaani hisia, akishika kitu fulani anajua ni mashine. Hata katika fedha aliyeona anatumiwa vidole vyake kubaini pesa ina thamani ya Shilingi ngapi,” anasema Kiranga.

Anaongeza kuwa wenye mahitaji maalumu, hasa wasioona ili kumpa mafunzo na aelewe ni lazima kumshikisha kwa mkono, na atakapopapasa ataelewa hii ni nyundo, mashine ya kukata chuma au mbao. 

"Muda wa kuwafundisha hadi waive ni mrefu, ili ashike. Hatua ya kwanza inabidi kwenda naye taratibu. Huwezi kuruka hatua ya kwanza hadi inayofuata kama ya awali hajaelewa, ila uwezo wao ni mkubwa sana wakishapapasa kitu kimoja wameshaelewa," anasema Kiranga.

Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Anthony Kasore, anasema: “Wenye mahitaji maalumu msiwafungie ndani, mlete mtoto, mzee, mama, kijana tumpe mafunzo. Lazima tuwe na taifa lenye ubunifu.”

Anasema VETA pia imekuja na mtaala maalumu kwa ajili ya kuwafunza watumishi wa ndani, mahausi geli ili kumudu kuwahudumia watoto na wazee pamoja na kuwaandaa kufanya kazi nje ya nchi.

Kadhalika, inasema inatarajiwa kuongeza idadi ya vituo vya mafunzo kutoka vilivyokuwapo awali 29 mwaka 2020 ili vifikie 143  mwakani, kutokana na kukua kwa mahitaji katika wilaya na mikoa yote nchini.

"VETA tumeleta vitu mbalimbali kuendana na nia ya maonyesho, kama vile huduma tunazotoa katika vyuo vyetu, kama eneo hitaji la mafunzo kwa wanaofanya kazi za ndani, tukiamini mtaala utawasaidiaWatanzania kupata mafunzo kuhudumia watoto, wazee.

"Mtu anafundishwa hadi kupika na tumeona kuna ambao wanahitaji kwenda nje ya nchi kufanya kazi kama hii, ili watambulike kuwa na vyeti tukaona vyema kuwa na ufundi huu ili wawe na ajira inayotambulika," anabainisha Kasore.

Anaongeza pia kuwa upo mtaala unaotoa mafunzo ya namna ya kutengeneza vifaa tiba, kwa kuanzia mkoani Mara na Geita, huku wakijikita kwa kuwa na mtaala wa watu wanaofanya kazi viwandani kwa kutumia mitambo ya kompyuta.

"Kozi hii imeanza Desemba mwaka jana, hasa kwa ambao wamemaliza vyuo kwa ngazi mbalimbali. Wawekezaji wanakuja nchini sasa hawatapata shida kupata watu wa kusimika mitambo na kuifanyia marekebisho, pia hatujaacha kuwatumia wabunifu," anaongeza.

Kasore anasema vipo vifaa saidizi kama vya kumenya viazi vya kilo moja kwa dakika, hususan kwa ambao wanakaanga magunia mengi kwenye biashara kila siku, badala ya kupoteza muda kwa kutumia visu.

Anasema wazazi na walezi pamoja na wazee waliostaafu, wafike VETA kujifunza ujuzi aina yeyote, ili kuwafanya wawe na shughuli ya kushughulisha mwili pia na kujiongeza kipato.

Boniface Kiyenze (64), ni mhitimu wa VETA, ameshiriki katika maonyesho ya mwaka huu, akisema kufanya useremala ndiyo maisha yake, akilea familia na wajukuu. 

"Nimeajiajiri natengeneza samani. Pale pale ninapoishi Dovya jijini Dar es Salaam, nina sehemu ya kufanya shughuli zangu napata wateja nauza na lea familia. Nina watoto wanne," anasema. 

Kiyenze ana wito kwa jamii isiwatenge watu wa kundi hilo, kwa kuwa wana mchango mkubwa katika ujenzi wa taifa na kujiinua kiuchumi wao binafsi.