Wapewa mbadala uchumi, wafanikiwa kunusuru mazalia ya samaki ufukweni

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:47 AM Oct 24 2024
Viongozi wa Shirika la Mwambao Coastal Community Network Tanzania, wakikabidhi fedha kwa wanachama wa vikundi vya Mkuba wilayani Mkinga vinavyotetea usalama wa bahari, Tanga hivi karibuni.
PICHA: BONIFACE GIDEON
Viongozi wa Shirika la Mwambao Coastal Community Network Tanzania, wakikabidhi fedha kwa wanachama wa vikundi vya Mkuba wilayani Mkinga vinavyotetea usalama wa bahari, Tanga hivi karibuni.

KUSHAMIRI shughuli zitokanazo na kuongezeka watu jirani na ufukweni, kunatafsiriwa kusababisha ongezeko la shughuli za kibinadamu, hata kuchangia kupungua uzalishaji samaki mahali hapo baharini.

Ndani yake, kikubwa zaidi ni uharibifu wa makazi ya samaki maarufu 'matumbawe' unaotokana na uvuvi haramu unaohusu ukataji miti ya mikoko na uchafuzi wa bahari ufukweni. 
 

Madhara mojawapo, ni katika uzalishaji samaki kama vile pweza walioko hatarini kutoweka, kutokana na ‘matumbawe.’ Ni hali inayowalazimu wadau wa maendeleo kujitokeza kuunga mkono juhudi za serikali kuhakikisha Uchumi wa Buluu.

 Aina ya uchumi unaotajwa kuleta matokeo chanya katika jamii hadi sasa, ni kuanzishwa kampeni zinazohamasisha wakazi waishio pwani, wahakikishe wanatunza rasilimali bahari ili kuongeza uzalishaji samaki mahali hapo.
 
 Hapo ndipo mmoja wa wadau katika ushirikiano wa umma na serikali (PPP), Shirika la Mwambao Coastal Community Network Tanzania, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kimataifa kama nchi za Norway, Asasi ya Eco Fish chini ya Jumuiya ya Ulaya (EU), The Nature Conversery (TNC) kwa ujumla wanafadhili kijiji cha Kigombe, wilayani Muheza.

 Kinachofanyika, wadau hao wawawezesha kiuchumi wakazi wanaoishi mwambao wa Bahari ya Hindi, wanaoziwezesha Jumuiya za Wavuvi na Mfuko wa Kutunza Bahari (MKUBA).

 Mpaka sasa wana boti mbili za ulinzi zimeshatolewa katika vijiji vya Boma Mahandakini na Boma, pia ikisaidia kuongeza wigo wa doria za ulinzi kwa vijiji tisa vya kata za Boma na Moa, zilizoko mpakani. 

Huko wanatoa elimu ya utunzaji rasilimali bahari na kuwawezesha kiuchumi, wakiwapatia mitaji na vitendea kazi vya kupunguza shughuli za kibinadamu zinazofanywa baharini, ili kuongeza ulinzi wa kukabili wahalifu baharini.
 
 Wilaya za Mkinga, Jiji la Tanga, Muheza na Pangani hadi majirani zao visiwani Zanzibar, ndio wanufaika wakubwa kwa kuwa shughuli zao nyingi za kiuchumi zinategemea bahari. 

Wakazi wa maeneo hayo wameanzisha mfuko wa kuhifadhi chombo cha baharini 'MKUBA', kinachowezesha kupata fedha, vitendea kazi kama boti na elimu ya utunzaji rasilimali za bahari, kupitia vikundi tajwa.
 
 BAHARINI KULIVYO

 Mratibu wa Shirika la Mwambao Coastal Community Network Tanzania Mkoa wa Tanga, Ahmad Salim Omar, anasema hali ya bahari ni mbaya. 

Anaorodhesha sababu zinajumuisha matukio ya uvuvi haramu, uharibifu wa makazi ya samaki, miti aina ya mikoko inazidi kukatwa kutokana na kuongezeka kwa matumizi yake katika jamii, uchafuzi wa fukwe za Bahari unaosababishwa na utupaji wa taka ngumu ambazo hugeuka kuwa sumu kwa viumbe bahari nalo ni janga jingine.
 
 Hivyo kwa kuliona hilo, anasema  wamelazimika kujitoa katika elimu ya utunzaji rasilimali za bahari na wakaunda mfuko maalumu wa kuhifadhi bahari unaoitwa MKUBA. 

Anasema, lengo la kuanzishwa mfuko huo ni kuwawezesha kiuchumi kwa kuwapatia mitaji na vitendea kazi wananchi wanaojiunga kwenye vikundi vya MKUBA wakiwapatia elimu ya utunzaji rasilimali za bahari na ujasiriamali wake.

 "Kupitia mfuko huu, wanachama wanapata elimu ya utunzaji rasilimali za bahari, elimu ya matumizi ya fedha na ujasiriamali, lakini mwisho kabisa tunawawezesha fedha na vitendea kazi.

“Lengo ni kuhamasisha jamii ya ukanda huu wa bahari wanapunguza shughuli za kibinadamu baharini, ili kuruhusu samaki wanazaliane kwa wingi," anasema Ahmad. 

Vilevile na ufafanuzi kwamba, wana kampeni ya kuhamasisha uchumi wa buluu, kupitia chombo hicho cha MKUBA na tayari anasema umeshaonyesha matokeo chanya, kwa zaidi ya wanufaika wake 4,422.

 Kwa mujibu wa Ahmad,mfuko huo wa s8 wa Kutunza Bahari 'MKUBA' wamenufaika kupitia fedha zinazotolewa kupitia vikundi 148 ambavyo vipo kwenye mradi huo huku zaidi ya Sh.248 zikitumika kuwainua kiuchumi wanachama wa vikundi vya 'MKUBA'.
 

· Boti la doria kwa ajili ya usalama wa baharini, wilayani Mkinga, Tanga. PICHA: MTANDAO.

"Lengo letu ni kuhakikisha wakazi wanaoishi Mwambao wa Bahari,wanapata elimu ya utunzaji wa rasilimali za bahari na kuwainua kiuchumi ili wapunguze shughuli za kiuchumi huko baharini, na kwa kufanikisha hili tumeamua kuwawezesha fedha kupitia vikundi.
 
Anasema wilaya ya Mkinga imepewa kipaumbele zaidi kutokana na kuwa na shughuli nyingi za kiuchumi zinategemea bahari, pia ipo mpakani na nchi zingine.

 "Halmashauri hii ya Mkinga tuna vijiji 12 kwenye programu za mradi huu wa MKUBA… pia kuna mradi mwingine unafadhiliwa na Ujerumani nao utakuja kwenye vijiji vingine," anasema Ahmad. 
 
 Anafafanua kuwa, wakazi wanaoishi mwambao wa baharini kutunza rasilimali za bahari, ili kuongeza uzalishaji wa samaki na kipato cha mwananchi mmoja mmoja.
 
 "Niwaombe wananchi wenzangu mtunze rasilimali za bahari, msikate miti hasa ya mikoko na kwa wavuvi msitumie baruti na sumu, ni hatari kwa afya zetu walaji na viumbe hai wa majini.

 â€œPia, tujitahidi kufanya usafi kwenye fukwe, ili tuifanye bahari kuwa safi muda wote. Tukifanya hivyo, itatusaidia kuongeza uzalishaji samaki," anaongeza Ahmad.
 
 WANUFAIKA WANAFUNGUKA

 Kassim Halfani, Mwenyekiti wa Jumuiya za Usimamizi wa Fukwe za Bahari (BMU) Wilaya ya Mkinga, anasema ujio wa mradi wa Mkuba umeongeza makusanyo ya ushuru kwa jumuiya hiyo na Halmashauri ya Mkinga.
 
 "Tokea umekuja mradi huu, mazao ya samaki yameongezeka, wavuvi wamekuwa wanavua samaki wengi na hasa pweza.

 â€œMvuvi mmoja kwa sasa anavua zaidi ya kilo 50 ya pweza na kilo ya pweza ni kati ya shilingi 7,500 na 7,000, wakati hapo awali mvuvi mmoja alikuwa anavua kilo mbili. Haya ni mapinduzi makubwa sana kwetu na tunajivunia kwa hilo," anatamka Kassim.

 Mwingine, Mohamed Ally, mkazi na mnufaika wa Mkuba, ana maelezo kwamba ni mageuzi yanayowafanya kuongeza uzalishaji samaki akiwa na ufafanuzi wake: 

 â€œKinamama, vijana na wazee wote wamepata mitaji na wanafanya biashara. 

Kiukweli imesaidia sana kuondoa wingi wa watu wanaofanya shughuli zao baharini, pia wengi wetu tulikuwa tunafanya kazi za uvuvi, ili tupate hela ya kula. 

 â€œKwa sasa, tunafanya kazi za kutuingizia kipato cha familia, kinachoweza kuleta maendeleo ya familia, ikiwamo kujenga nyumba nzuri ya kisasa," anatamka Ally
 
 KUTOKA HALMASHAURI 

 Ofisa Uvuvi wa Halmshauri ya Wilaya ya Mkinga, Ezra Katete, anasema awali kabla ya mradi huo, hali ilikuwa ngumu zaidi hususani kwenye ulinzi na doria za baharini.
 
 "Mdani ya muda mfupi baada ya ujio wa mradi huu, umeleta matokeo makubwa. Tumefanikiwa kupata boti za ulinzi na kwa kushirikiana na Jeshi la KMKM (Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo) tumeimarisha ulinzi baharini na kupambana na wavuvi haramu…

 â€œTayari tumeshakamata baadhi yao, lengo tunataka tuone matokeo chanya kwa jamii yetu inayoishi ukanda wa bahari," anasema Ofisa Uvuvi Ezra.

 Anasifu juhudi za kutunza rasilimali za bahari na kuwainua wananchi kiuchumi zinazoendelea kuiunga mkono serikali katika kufikia uchumi wa buluu.