Vita vya DRC Ukanda Maziwa Makuu hatarini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:05 AM Feb 05 2025
Waasi wa M23 wanaoendeleza vita DRC
Picha: Mtandao
Waasi wa M23 wanaoendeleza vita DRC

NCHINI Congo DRC ni vilio, watu duniani wakiangalia runinga machozi yanawatoka wakisikitika ni miaka mingi zaidi ya 20 nchi hiyo imejaa ghasia na hata leo hali ni tete.

Waasi wa M23 wa Congo wanatishia amani ya ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Maziwa Makuu na kuongeza hofu.

ATHARI KIKANDA 

Mataifa jirani yanaugulia kwa sababu mashambulizi yanasababisha mamilioni ya wakimbizi kutoka maeneo yote ya Kivu Kusini na Goma kutawanyika Afrika Mashariki. 

Wakongo hao wanakikimbilia Rwanda, Uganda, Burundi, Tanzania na Kenya.

Katika kujiokoa kila kitu kinavuka mipaka kuanzia silaha ndogo na kubwa yote hayo yakitishia usalama. Uwezekano wa kuongezeka uhalifu na uporaji na hata mauaji kutumia silaha.

Vita vinavuruga uchumi eneo la Maziwa Mkuu. Jambo lisilopingika ni kushuka shughuli za kibiashara kutokana na kukosa usalama, kwenye makazi, vituo vya kuuza na kununua miundombinu ya usafirishaji.

Uharibifu wa mazingira hasa kukata miti na kuvamia mapori ili kupata makazi na shughuli za wakimbizi ni mambo yasiyokwepeka ukanda wa nchi jirani.

Vita vinavuruga usafiri wa watu pamoja na bidhaa hasa mipakani hata angani kwa vile upo uwezekano wa kushambuliwa.

Jamii wenyeji kukosa amani na utulivu kutokana na  kufurika kwa watu wageni kwenye makazi au maeneo yao.

Mwaka 2025 umeanza vibaya DRC  kutokana na ubabe wa waasi hao ambao wameua watu zaidi ya 700.

Wanatamba kuwa watasonga mbele  tena wakiapa kupigana hadi kutwaa mji mkuu wa Kinshasa.

Waasi wakidaiwa kuungwa mkono na Rwanda wanatangaza kuendeleza vita vyao hadi mji mkuu Kinshasa, ambako Rais  Tshisekedi anatoa wito wa kuajiri wanajeshi wapya katika kukabili vita dhidi yao.

Mji wa Goma kuangukia tena mikononi mwa waasi wa  M23 kunaongeza  mawimbi ya mshtuko, hofu na wasiwasi katika eneo la Maziwa Makuu na hatari ya kuzusha vita vinavyoweza kuenea ukanda mzima. 

Wacongo wanazidi kuteseka wakikumbuka vita vya mwishoni mwa miaka ya 1990 na mwanzoni mwa  2000 ambapo wanajeshi wa mataifa saba ya Afrika yaliingilia kati na kurejesha amani.

Vita hivyo vilisababisha  Wakongo milioni 5.4 kuuawa.

Mapambano hayo yanayoendelea yanatisha hasa kwa sababu M23 imekuwa ikiendeleza uasi huo kwa miaka mingi ikidaiwa inaungwa mkono na Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF), lengo likiwa kutetea maslahi ya Rwanda.

Kuna madai kuwa kati ya wanajeshi 6,000 wa M23, kuna takriban wanajeshi 4,000 wa Rwanda.

Aidha, upo ushahidi kutoka kwa uchunguzi wa Umoja wa Mataifa kwamba M23 inapokea msaada kutoka Uganda. 

Ripoti zinaonyesha kuwa wanajeshi wa Kongo, wanamgambo wanaoungwa mkono na serikali wanaojulikana kwa jina la Wazalendo, na mamluki wa kigeni wamejisalimisha kwa wanajeshi wa RDF nchini DRC.

Mkakati na mpango kabambe wa kuiteka Goma, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini wenye utajiri mkubwa wa madini mashariki mwa DRC, umefanikiwa na sasa waasi wanaendelea kukoleza mashambulizi  waliyoyaanzisha tangu 2022 wakikamata na kudhibiti eneo la mashariki mwa Congo.

Hatua hiyo inahusishwa na juhudi za kuanzisha utawala mwingine wa eneo huru lisilofungamana na serikali ya Kinshasa, kwa sababu unayahusu maeneo yanayodhibitiwa na M23 wakilenga upanuzi wa miradi ya kuchimba madini. 

Hii inamaanisha kwamba kundi la waasi na wanaowaunga mkono wana malengo ya muda mrefu katika kushikilia na kuongeza zaidi himaya yao na kufanikisha udhibiti wao wa kijeshi.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN) zaidi ya watu 500,000 wamekimbia makazi yao tangu kuanza mwaka huu, wakati maelfu wakifikishwa hospitali ambazo zimezidiwa na majeruhi, wengi wao wakiwa raia. 

Biashara zinakwama maduka hadi kwenye uzalishaji kumefungwa kutokana na mapigano makali ambayo pia yanaua walinda amani 17 wakiwamo kutoka mataifa ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wanaoshiriki Misheni ya Umoja wa Mataifa ya Kudhibiti Utulivu DRC (MONUSCO).

Machi 2024, Umoja wa Mataifa uliripoti kwamba idadi ya wakimbizi wa ndani wa  DRC ilifikia milioni 7.2 ukisema ni moja ya idadi kubwa zaidi duniani ambayo haijawahi kutokea.

UN inakadiria kuwa tangu 1996, vita mashariki mwa DRC vimesababisha takriban vifo milioni sita.