Usiyoyajua wapinzani wa Simba, Yanga CAF

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:45 AM Oct 14 2024
Kikosi cha MC Alger ya Algeria ambacho kinatarajia kushiriki mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika. MC Alger iko Kundi A pamoja na wawakilishi wa Tanzania Bara, Yanga.
PICHA: MTANDAO
Kikosi cha MC Alger ya Algeria ambacho kinatarajia kushiriki mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika. MC Alger iko Kundi A pamoja na wawakilishi wa Tanzania Bara, Yanga.

BAADA ya kufanyika kwa droo ya hatua ya makundi, tayari wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya kimataifa Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika wameanza maandalizi.

Yanga imepangwa Kundi A katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Al Hilal (Sudan) na MC Alger ya Algeria huku  Simba ambayo itacheza mashindano ya Kombe la Shirikisho iko Kundi B na Bravo do Maquis ya Angola, CS Coastantine ya Algeria na CS Sfaxien ya Tunisia.

Si wengi wanaojua njia gani zimepita timu hizo hadi kutinga hatua hiyo, lakini pia rekodi zao katika michuano wanayocheza.

Pia hakuna anayejua vyema maendeleo yao kwenye Ligi Kuu za nchi zao katika msimu huu unaondelea.

Mwandishi wa makala haya, anakuletea kila kitu ambacho kitakufanya uzijue timu hizi zimefikaje hatua ya makundi, rekodi zao kwenye michuano na msimu huu zifanya nini kwenye ligi za nchini zao.

 

TP MAZEMBE 

 

Ndiyo timu yenye rekodi nzuri zaidi katika Kundi A, ambalo lina wawakilishi wa Tanzania, Yanga.

Imetwaa taji hilo la Ligi ya Mabingwa mara tano, ikifanya hivyo 1967, 1968, wakati huo likiitwa Kombe la Klabu Bingwa Afrika, 2009, 2010 na 2015.

Imefika hatua ya fainali mara mbili, 1969 na 1970, imecheza nusu fainali ya ligi hiyo mara nne (2002, 2012, 2014 na 2018/19), huku ikifanikiwa kucheza hatua ya robo fainali mara mbili, 2018/2019 na 2019/2020.

Timu hiyo imetinga hatua ya makundi ilicheza mechi ya raundi ya kwanza dhidi ya Red Arrows ya Zambia, ikishinda mabao 2-0 ugenini, na kushinda tena nyumbani mabao 2-1, hivyo kutinga makundi kwa jumla ya magoli 4-1.

Haikuwa kwenye kiwango kizuri misimu miwili iliyopita, lakini imeboresha kikosi chake msimu huu kwa kufanya usajili bora na kurejea kule ilikokuzoea.

Mpaka sasa imecheza mchezo mmoja tu kwenye ligi ya nchini kwao, Oktoba 5, mwaka huu dhidi ya Malole na kulazimishwa sare ya bao 1-1 ikiwa nyumbani.

 

AL HILAL 

Jina lake kamili inaitwa, Al Hilal Omdurman yenye maskani yake nchini Sudan. Ni moja kati ya timu zenye rekodi nzuri ya kucheza mara nyingi hatua za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Imecheza Ligi ya Mabingwa Afrika mara 39, tangu ikiitwa Klabu Bingwa Afrika, lakini mara zote haijawahi kutwaa taji hilo.

Hata hivyo, ina rekodi ya kufika fainali mara mbili (1987 na 1992), pia ikitoa mfungaji bora Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2011, wakati straika wa timu hiyo, Edward Sadomba, raia wa Zimbabwe, alipopachika mabao saba na kutwaa kiatu cha dhahabu.

Imetinga nusu fainali mara nne, robo fainali mara mbili, ikiishia hatua ya makundi mara tisa.

Msimu huu imeweka rekodi ya kutinga hatua ya makundi mara sita mfululizo, mara baada ya kuichapa Al Ahly Benghazi ya Libya ikicheza ugenini na sare ya bao 1-1 ikicheza Sudan Kusini.

Kwa misimu miwili sasa haichezi ligi nyumbani kwao kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe, badala yake inacheza ligi nchini Mauritania na imeshinda michezo yote miwili iliyokipiga nchini humo, ikiichapa Inter Noakchot mabao mabao 4-1, na magoli 5-0 ikiwaadhibu Nzidane.

 

MC ALGER

 

Inaitwa Mouloudia Club d'Alger, kifupi MC Alger ya Algeria. Imeshawahi kutwaa ubingwa huo, lakini ikiwa ni mwaka 1976, ikifika hatua ya robo fainali mara tatu, 1977, 1980 na 202, ikishiriki michuano hiyo mara tisa.

Imeanza michuano hiyo raundi za awali kama Yanga, ikiiondoka Watanga FC ya Libya kwa jumla ya mabao 4-0, ikishinda mabao 2-0 nyumbani na na ushindi kama huo ugenini.

Timu hiyo inakamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini Algeria, ikicheza michezo minne, ikishinda miwili na sare mbili, ikiwa na pointi nane, nyuma ya Olympique Akbou, inayoongoza kwa pointi tisa.

 

BRAVOS DO MAQIS

 

Hawa ni wawakilishi wa Angola katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, wakiwa kundi moja ya Simba.

Haina rekodi yoyote ya kuvutia kwenye soka la nchi hiyo, lakini imefanikiwa kucheza michuano hiyo kwa kutwaa Kombe la FA nchini humo msimu uliomalizika.

Njia iliyopitia ni kuiondoka Coastal Union ya Tanzania kwa kuifunga mabao 3-0, iliyotapata ikicheza nyumbani, kabla ya kulazimishwa suluhu waliporudiana hapa nchini kwenye hatua ya raundi za awali.

Raundi ya kwanza ilicheza na FC Lupopo ya DR Congo, ikishinda bao 1-0 nyumbani, kabla ya kwenda kushinda tena ugenini kwa magoli 2-1.

Kwenye ligi nchini mwake inakamata nafasi ya tisa, ikicheza mechi nne, kushinda moma, sare mbili, ikipoteza moja, mchezo wa mwisho ikipigwa mabao 2-0 dhidi ya Petro de Luanda.

 

CS COSTATINE

 

Ni moja ya timu ambazo kwa sasa zinasumbua kwenye ligi ya Algeria, ingawa haina rekodi nzuri sana katika mashindano ya kimataifa.

Imecheza Kombe la Shirikisho mara mbili na zote ikiishia raundi ya pili, hivyo hii ni mara ya kwanza kutinga hatua ya makundi, ikiwa pamoja na Simba.

Ilianza mechi za awali kwa kuichapa, Polisi ya Rwanda mabao 2-0, na ikashinda tena ugenini mabao 2-1, hivyo kutinga raundi ya kwanza, ikakutana na Nsoatreman ya Ghana na kuinyuka mabao 2-0 ikicheza ugenini, ikashinda tena bao 1-0 ugenini na kutinga makundi. Inakamata nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini mwao ikiwa na pointi sita kwa michezo minne iliyocheza.

 

CS SFAXIEN

 

Imepangwa Kundi A katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, CS Sfaxien ndiyo timu yenye rekodi nzuri zaidi kuliko zote.

Imetwaa kombe hilo mara nne, mara moja wakati likiitwa Kombe la Washindi Afrika.

Ilianza kulitwaa 1998, baadaye ikafanya hivyo 2007, 2008, na 2013, wakati limeshabadilishwa jina la kuitwa Kombe la Shirikisho. Ilianza moja kwa moja kucheza raundi ya kwanza kama Simba, ikiichapa Rukinzo ya Burundi bao 1-0 ikiwa ugenini, na kushinda tena nyumbani bao 1-0, kabla ya kutinga makundi.

Kwenye Ligi Kuu nchini Tunisia ipo nafasi ya sita, ikicheza mechi nne, ikiwa na pointi saba mpaka sasa.