MATUMIZI ya protini kama dagaa na soya kulisha wanyama yanaongezeka. Hata hivyo, vyakula hivyo pia hutumiwa na binadamu, jambo linaloongeza ushindani, mahitaji na gharama sokoni.
Ubunifu ni njia mojawapo inayoweza kutumiwa kupata bidhaa hizo kama jamii itafundishwa jinsi ya kutumia malighafi zilizopo ili kupata protini na vyakula vingine vya kulisha wanyama.
Ubunifu upo wa aina nyingi, lakini kwenye eneo la protini za mifugo Juma Masanja, anaeleza namna ya kuzalisha protini kwa kutumia maganda ya matunda na mabaki ya vyakula kwa ajili ya wanyama na kuku ili kuboresha afya zao.
Anasema chakula hicho huzalishwa kwa kutumia maganda ya matunda na vyakula vinavyobaki au makombo kuanzia ugali, maharage, wali na mboga ambavyo baada ya kukusanywa na kuwekwa mahali kwa muda mfugaji anapata funza wa kulisha wanyama.
Anasema miongoni mwa matunda ni matikiti maji, mafenesi, maembe, ndizi, maparachichi, lakini pia maganda ya viazi, mabaki ya mboga za majani na makombo.
Mtaalamu huyo wa kuzalisha funza hao Masanja kutoka Kituo cha Sauti ya Jamii Kipunguni jijini Dar es Salaam, anazungumza na Nipashe hivi karibuni akitaja mbinu anazotumia kufikia lengo hilo.
Ni katika mafunzo ya jinsi ya kutumia taka hizo kwa tija yanayotolewa na kituo hicho kwa vikundi vya uzalishaji mali vya kata za Majohe na Kivule ili kuondoa umaskini na kuboresha maisha.
Masanja anasema, ili kupata wadudu hao, malighafi hizo zinakusanywa, kujazwa katika ndoo ya lita 20 na kuachwa kwa wiki tatu ili wadudu hao wapatikane. "Baada ya siku 21, wadudu waitwao 'black soldiers' wamezalishwa na wako tayari kuvunwa kwa ajili ya kulisha ng'ombe, nguruwe au kuku. Wanaprotini nyingi zinazowafanya wanyama kunenepa," anasema Masanja.
Mtaalamu huyo anafafanua kuwa, kilo 100 za taka hizo, zinaweza kutoa kilo moja ya wadudu hao, na kwamba ndoo moja ya taka inavunwa mara tatu kila baada ya siku 21.
Anaeleza kuwa, wanaweza kukaushwa au kulishwa mifugo wakiwa wabichi. Masanja anasema, kilo moja ya wadudu hao inachanganywa katika kilo 20 za pumba wakiwa wabichi au wakawa wamekaushwa na kuwalisha ng'ombe, nguruwe au kuku. Wadudu hawa wanavunwa mara tatu kila baada ya siku 21, kabla ya kubadilisha taka.
Vilevile, taka zikishamaliza muda wake wa kuzalisha wadudu, zinatumika ni mbolea," anasema. Anaeleza kuwa, kwa kutumia ubunifu huo, kituo kinapunguza uchafuzi wa mazingira kwenye jamii, hasa kupitia taka ambazo wanazizalisha wadudu hao, kwa ajili ya lishe ya mifugo. Katika maelezo yake zaidi, anasema wameamua kuingiza taka kwenye mnyororo wa thamani, kwa kuzitumia kuandaa chakula ambacho kinajenga afya ya mifugo, lakini pia kutumika kama mbolea kwenye bustani, badala ya kuzitupa.
"Wakati tunaanza kuzalisha wadudu hawa, tulikuwa tunauza kilo moja kwa shilingi 10,000, lakini kwa sasa tunauza kilo moja kwa shilingi 5,000 ili kuvutia wateja wengi zaidi," anasema. Aidha, Masanja anasema;
"Nilipata elimu kutoka Taasisi ya Utafiti na Matibabu Afrika (AMREF) ya jinsi ya kuutumia taka kuzalisha funza wenye virutubisho, kwa ajili ya ya lishe kwa mifugo. Nimeileta kuingiza taka katika mnyororo wa thamani kwa kuzitumia kupata chakula cha wanyama," anasema. Beatrice Oswald kutoka Kivule anazungumzia mafunzo hayo, akisema yana manufaa mengi ikiwamo kupunguza uchafuzi wa mazingira, iwapo utazingatiwa na kila mdau.
"Kwanza unasaidia usafi wa mazingira, kwani mara nyingi taka za majumbani mwetu zinatokana matunda na hata mabaki ya chakula,” anasema Beatrice. Anasema badala ya kutupa taka hizo, sasa atazitumia kuzalisha wadudu hao na pia kwa ajili ya mbolea ambayo ataitumia katika bustani yake ya mboga, kwa kuwa haina gharama.
"Unaweza kwenda kwa mtu kuhitaji mbolea ya samadi ukauziwa, lakini hii ya maganda ya matunda hawezi kuuziwa, kwani hizo ni taka.
Hivyo, ninakwenda kutumia kwa mambo mawili, kuzalisha wadudu na pia kupata mbolea," anasema. Beatrice anasema, elimu aliopata haitaishia kwake, bali taipeleka kwa wenzake ili nao waone umuhimu wa kuzalisha wadudu, kwa ajili ya kuboresha afya ya mifugo yao.
Anafafanua kuwa, wamefundishwa kwamba kilo moja ya wadudu hao inauzwa Sh. 5,000, na kwamba mtu anaweza kufanya biashara ya kuwavuna na kuuzia wafugaji au kuwalisha mifugo wake na kutumia kama mbolea.
Amina Omary kutoka Majohe anasema, licha ya kuhisi kinyaa baada ya kuona wadudu hao, itabidi abadilishe mtazamo ili aende kulingana na fursa za kiuchumi zilizoko. Anasema, ataendana na mazingira, asipitwe na wakati, kwa kuwa maisha yanakwenda mbio na ubunifu katika vitu mbalimbali unazidi kuongezeka kila kukicha.
Mjasiriamali huyo anasema, kwa kutumia malighafi hizo ambazo ni nyingi na rahisi kupatikana sokoni na hata nyumbani, usafi wa mazingira utaimarika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED