WIKI hii inahesabika neema mpya katika mafanikio ya utawala wake Rais Dk. Samia Suluhu, akiingiza rekodi mpya ya maendeleo, pale unapohusishwa mradi mkubwa wa nchini, njia ya usafiri ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) uliokuwa unalega.
Mwanzo wa wazo la ujenzi ulikuwa mwaka 1968, ukaanza miaka miwili baadaye, kisha huduma zikaanza kufanyika, 1976.
Hapo kuna zao la ubunifu na urafiki kati ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, swahiba wake kisiasa, kijamii na kiitikadi, jirani Rais Kenneth Kaunda wa Zambia na komredi wao, Mao Tse Tung wa China.
Serikali ya Mao Tse Tung, ilitoa mkopo usio na riba kwa mradi huo wa marafiki, wajenzi wakitoka China. Hivyo, kinachofanyika sasa katika Serikali ya Awamu ya Sita, ni mwendelezo wa maono yaliyoibuliwa na Nyerere, miaka saba baada ya uhuru, leo ikielekea mwaka wa 67 wa maadhimisho hayo.
Ni mtazamo uleule uliowasilishwa hivi karibuni katika safu hii, Serikali ya Awamu ya Sita, inavyoendeleza mashirika ya umma, kwa mwongozo wa Mwalimu Nyerere, ila mahitaji ya sasa.
Hadi sasa nchini kuna miradi mikubwa ya namna hiyo inayoendelezwa ya Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere, ambalo ni wazo la Baba wa Taifa, aina yake ya fikra ikiendelezwa katika reli nchini.
Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) ulioasisiwa kwa maono ya Serikali ya Awamu ya Nne, wote wakiwa waumini wa itikadi ya serikali ya Nyerere na dira yake.
Wakati mradi wa reli ya TAZARA ilianza kutumika mwaka 1976, ulikuja na sifa iliyoko leo ya mradi unaondelezwa kwa jina la Reli ya Kisasa (SGR), ambayo upana wa reli unazidi ule mkongwe Reli ya Kati ya TRC.
Pia, ujenzi wa sakafu yake imetandikwa nguzo za zege na kokoto nyingi, tofauti na ile kongwe yenye nguzo chuma ambayo reli yake pia nyembamba kulinganisha na SGR inayotajwa imara na salama zaidi; Reli ya TRC ilijengwa mwaka 1905 na kazi ya upimaji ilianza 1894, katika Utawala wa Koloni la Kijerumani.
Wiki hii China, Tanzania na Zambia zimetia saini makubaliano ya awali kuifanyia matengenezo reli ya Tanzania hadi Zambia kukilengwa kuboresha usafirishaji katika ukanda huo wenye utajiri wa rasilimali.
Wakati mkataba wa awali ulihusisha wazee; Mao Tse Tung, Nyerere na Kaunda, wa sasa ni marais wa Zambia, Hakainde Hichilema na Dk. Samia, na mwenyeji Rais Xi Jinping wa China, wote wakihudhuria Mkutano wa Ushirikiano Kati ya Afrika na China.
Mradi wa kwanza wa TAZARA, reli yenye urefu wa kilomita 1,860, ulijengwa kati ya mwaka 1970 na 1975 kwa mkopo usio na riba kutoka China, malengo ni kusafirisha mizigo kutoka migodi ya madini ya shaba na kobalti ya Zambia hadi bandarini, Dar es Salaam, Tanzania.
Ujenzi huo ulihusisha madaraja mengi, njia za chini na mapango, ikijumuisha wafanyakazi wa China zaidi ya 20,000 na wenyeji wa nchi hizo mbili.
Mradi wa TAZARA unaunganisha huduma ya abiria na mizigo kati ya bandari ya Dar es Salaam na kituo cha New Kapiri Mposhi, iliyopo kwenye njia ya reli kati ya Lusaka na Kitwe, ukanda wa shaba wa Zambia, ukichangia uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizo.
Kisiasa, ililenga usafirishaji shaba ya Zambia wakikwepa bandari za Afrika Kusini iliyokuwa na serikali ya kibaguzi, pia Msumbiji, ilipokuwa koloni la Ureno.
China ikaunga mkono kwa kuwekeza katika uhusiano na msimamo huo wa mataifa huru ya Afrika, ikajitolea kudhamini mradi uliowezesha Zambia njia nyingine ya kufikia bahari.
Reli hiyo inatajwa ilipoanza kazi mwaka 1976, ilikuwa na vichwa 120 na mabehewa zaidi ya 2,000, sasa zinakadiriwa ni wastani wa vichwa 30 na mabehewa 100, huku hali ya reli na mtaji wa shirika si mzuri.
Ni njia inayopita kati ya misitu mapori, mapango makubwa na ya kuvutia nchini katika mikoa ya Kusini, Tanzania.
VITUO MUHIMU TAZARA
• Dar es Salaam
• Kidatu (kiungo na Shirika ya Reli Tanzania kwenda Kilosa na Dodoma)
• Ifakara
• Mlimba
• Makambako
• Mbeya
• Tunduma (Tanzania)
• Kasama (Zambia)
• Mpika
• Serenje
• New Kapiri Mposhi - kiungo na reli ya Zambia
SAMIA KIKAONI
Rais Dk. Samia yuko China, kwenye mkutano uliofunguliwa juzi na Rais Xi Jinping, mwenyeji wa viongozi 25 wa Afrika, hoja yake ni kuwashawishi Waafrika wanunue bidhaa nyingi za nchini mwake, kwa ahadi ya kuwapa misaada na uwekezaji zaidi.
China, inataka kupunguza uwekezaji kwingine na kuboresha uhusiano wake na nchi zinazoendelea ikiwano mikopo, pia kujikita kuwekeza kwenye miradi midogo, badala ya mikubwa ya miundombinu.
Hadi sasa kampuni nyingi za China zimewekeza katika kandarasi za ujenzi nchini, pia bidhaa zake za matumizi ya kawaida zimetawala soko nchini.
Rais Dk. Samia, kama inavyozoeleka katika vikao vingi vya maendeleo kimataifa anavyohudhuria, akatarajiwa kuhutubia mkutano huo wa Tisa, kunatarajiwa kutoa mwelekeo wa ushirikiano kati ya China na Afrika, hasa baada ya janga la corona.
Pia, unafanyika wakati ambapo msuguano wa kisiasa unazidi kuongezeka katika ngazi ya kimataifa, mathalani vita vya Russia na Ukraine, pia nyingine nyingi Afrika kama mapigano ya ndani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Viongozi wa Afrika, nao wanatafuta suluhisho la haraka la madeni yanayozidi kuongezeka barani humo, uwekezaji kuhakikishiwa miradi iliyoahidiwa katika mkutano wa mwaka 2021, Dakar, Senegal.
BANDARI KAVU
Mnamo Oktoba mwaka jana, Rais Dk. Samia, akatangazwa kutengwa ardhi ya hekta 20 kwa jirani yake Zambia, eneo la Kwala mkoani Pwani, kujengea bandari kavu, kufufua mazingira ya kibiashara na usafiri wa reli, TAZARA.
Ni hatua iliyochukuliwa, huku utendaji wa reli ya TAZARA inayomilikiwa na pande zote mbili, ulega, Rais akitaja shabaha ni kuharakisha usafirishaji mizigo inayopitia Bandari ya Dar es Salaam na kusafirishwa kwa barabara hadi sehemu mbalimbali nchini Zambia.
Vilevile, hivi karibuni serikali ilizindua bandari ilyopanuliwa ziwani na barabara kujengwa mkoani Rukwa, inayounganisha usafiri kati ya Tanzania na DRC.
Hilo linatokea, huku takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Mamlaka ya Mapato (TRA) mwaka jana, zikaonyesha mwaka 2022, Tanzania iliingiza nchini bidhaa za Zambia zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 91, huku kiwango ilichosafirisha kwenda huko ni dola milioni 80.
Mwaka 2018, Dk. Samia akiwa Makamu wa Rais, serikali ilizindua ujenzi wa Bandari kavu Inyala, katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, akiufafanua ni nguzo muhimu ya ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na nchi zinazopakana nazo upande wa Nyanda za Juu Kusini, ikiwamo Malawi na Zambia.
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, kwenye ziara ya Makamu wa Rais Dk. Samia, alipotembelea Bandari ya Itungi katika Ziwa Nyasa, kukagua ujenzi wa meli ya MV Mbeya II.
Makalla akasema ujenzi wa bandari kavu Inyala ulitegemewa kufanya mageuzi ya usafirishaji mizigo nchini, kupitia reli ya TAZARA ambayo ina gharama nafuu, kuliko barabara inayotumika zaidi sasa.
"Makamu wa Rais (Dk. Samia wakati huo), ujenzi wa bandari kavu Inyala ni nguzo muhimu katika ukuaji wa kiuchumi wa mkoa wa Mbeya na taifa kwa ujumla, kwani itasaidia kusogeza huduma za bandari toka Dar es Salaam hadi Mbeya hali itakayowapunzia gharama za usafiri wateja wetu wa nchi za Malawi, Zambia na Kongo," akatamka Makalla, miaka sita iloyopita.
UMEME TZ KUTUA ZAMBIA
Mwaka jana serikali ilitangaza mradi wa upatikanaji umeme mikoa mitano nchini, kutoka Bwawa la Mwalimu Nyerere, uliambatana na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya Kilovoti 400 kutoka Iringa- Zambia (TAZA) na ulianza kutekelezwa Januari mwaka jana, kukitarajiwa kukamilika Janauri mwakani.
Aliyekuwa Waziri wa Nishati, January Makamba, akasema kuna eneo panajengwa Kituo cha Kupoza umeme eneo la mpakani Tunduma wilayani Momba, mkoa wa Songwe na kuna vingine vinne kama hivyo viliarajiwa kujengwa.
Mratibu wa Mradi huo. Mhandisi Elias Makunga, akasema ungetekelezwa kwa Sh. trilioni 1.4 ambazo serikali ilikuwa nazo na itakuwa kiunganishi cha kwanza cha umeme wa juu kati ya nchi Wanachama wa Kusini mwaka Afrika (SAPP)na Nchi Wanachama wa Mashariki mwa Afrika (EAPP), hali itakayochagiza biashara ya umeme, kwani Tanzania itaweza kununua umeme nje ya nchi pale panapokuwa na upungufu, pia itaweza kuuza nje pale inakuwa na ziada.
VYAKULA KUUZWA
Mnamo Juni mwaka huu, Tanzania imeingia makubaliano ya kuuzia Zambia tani 650,000 za mahindi, kusaidia taifa hilo kutokana na ukame unaoikumba. Kwa mujibu wa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, mkataba huo unatekelezwa kwa kipindi cha miezi nane na utaiingizia Tanzania Dola Milioni 250 sawa na Sh. bilioni 650 za Kitanzania. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, akaihakikishia Zambia kuwa mahindi hayo watayapata kwa wakati bila vikwazo vyovyote.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED