TGNP na kampeni nyumba kwa nyumba kuhamasisha kutoa maoni dira 2050

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 07:11 AM Sep 04 2024
 Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Lihundi
Picha:Mtandao
Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Lihundi

MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP), haupo nyuma kupinga ukatili wa kijinsia mara hii ikipenyeza ajenda kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025-2050, kulifanikisha ajenda usawa.

Mtandoa huo ukitumia tamasha la siku tatu lililotamatika hivi karibuni wilayani Kondoa Dodoma kufikisha ujumbe serikalini ili dira ijayo itokomeze ukatili wa kijinsia. Katika tamasha hilo, Ofisa Mwandamizi wa Idara ya Utafiti na Uchambuzi wa Mtandao huo, Zainabu Mmari, anasema uchambuzi wa mtandao umebaini Dira ya Maendeleo 2025 inayomalizika wananchi wengi hawakuifahamu.

Anafafanua kuwa wengi hawakushirikishwa katika mchakato wa kutoa maoni na pia hawakuielewa wakati wa utekelezaji wake lakini safari hii kasoro hiyo haipo. Anasema dira 2025 kuna upungufu mkubwa wa kijinsia ambao umejitokeza maeneo matano yaliyowekwa kama vipaumbele vya dira. “Upungufu uliokuwapo ni wananchi wengi kukosa uelewa kwamba hiki tunachokifanya ndicho kinakwenda kutekeleza dira kufikia yale maisha bora tuliyoambiwa.” 

 “Hivyo, mwisho wa siku tulikuwa tunatekeleza bila kuelewa tunafanya nini ili kufikia malengo tuliyoahidiwa,” anasema Zainabu. Anafafanua kuwa katika tamasha hilo wameangalia pia kwa kiasi gani makundi yote katika jamii hususani wanawake na wale wanaoishi pembezoni walipata fursa ya kushirikishwa katika mchakato wa maandalizi ya dira. 

Anasema licha ya kwamba kuna mafanikio yaliyofikiwa katika maeneo kadhaa, kuna udhaifu mkubwa na pengo la kijinsia ambalo limejitokeza katika maeneo matano ambayo yaliwekwa kama vipaumbele vya dira akitolea mfano maeneo ya kijinsia hayakupewa kipaumbele kikubwa.

 Anasema changamoto nyingine waliyoibaini ni kutokuwapo kwa viashiria vya kupima dira hiyo hasa kwenye masuala ya jinsia. Zainabu anasema kutokana na changamoto hiyo kubwa TGNP inaendelea kuweka mkazo na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kutoa maoni katika dira inayoandaliwa.

 “Mpaka sasa tumeelimisha wananchi wengi kuelewa dira inayomalizika, lakini kuhimiza kuweka maoni yao kwenye dira mpya pia kufuatilia kuona kuwa  yanachukuliwa ili kuwa na Tanzania wanayoitaka katika miaka mingine 25 inayokuja itakapofika 2050,” anasema Zainabu. Mratibu wa Vituo vya Taarifa na Maarifa vinavyoendeshwa kwa pamoja na wananchi, asasi za kiraia na TGNP  kutoka Kata ya Ukenyenge Mkoa wa Shinyanya, Fredina Saidi, anasema namna walivyoshirikishwa kwenye kutoa maoni  wanajamii wamejengewa ufahamu na kujamini. 

Anasema kupitia ushirikishwaji unaofanywa na TGNP wameelewa namna gani wanaweza wakatoa maoni hususani mambo ambayo yanawahusu kwenye, usawa wa kijinsia, afya, maji, elimu miundombinu pamoja na usalama wa watu wote.

“Sisi wanajamii tuna jukumu kubwa la kuangalia matatizo na upungufu ambao tunao, tutoe maoni kuhusu mambo gani tunatamani yawepo ndani ya mpango huo mkubwa wa kimaendeleo,” anasema.

 UELEWA WANANCHI

Katika tamasha hilo, Nipashe inafanya mazungumzo na wakazi wilayani huko na kubaini wengi wao hawana uelewa  kuhusu dira ya taifa ya maendeleo na ukatili wa kijinsia, pia maadhimio ya miaka 30 ya mkutano wa Beijing.

Viktoria Ikandilo anaiomba serikali kuongeza nguvu kukabili vitendo hivyo ikiwamo kutoa elimu na kuweka sheria kali. 

“Kesi nyingi zinamalizwa kifamilia kwa kuwa kuna jamii hazina uwelewa wa masuala ya ukatili wa kijinsia.  

“Ndiyo maana kuna watoto wengi wa mitaani, wameathirika kisaikolojia, wimbi kubwa la ulawiti kwa kuwa ni vitendo vinavyoanzia zaidi majumbani na wazazi wengi hawakemei kwa sababu hawajui madhara yake,” anasema.

 Anasema tamasha hilo limeleta tija katika kuelimisha na kuhamasisha jamii, serikali na wadau kuwekeza nguvu na kutoa adhabu kali. 

Aidha, anasema: “Hatujui nini maana ya dira ya maendeleo ya taifa, tunaona meseji kwenye simu tunazifuta hatujui inamaanisha nini tunaona kama zile za matapeli tu. 

Anasema tamasha hilo litaleta tija katika kuelimisha na kuhamasisha jamii, serikali na wadau kuwekeza nguvu na kutoa adhabu kali. 

Mkazi mwingine Veronika Nganguli anasema tamasha hilo litahamasisha mwamko kwa makundi yote ili yatoe maoni kwenye diara ya taifa 2050. 

“Hasa ni kutoa maoni katika masuala ya nafasi za uongozi, uchumi, afya, elimu pamoja na kukumbushia malengo ya mkutano wa Beijing uliokuwa umelengea kueneza vuguvugu la usawa kati ya wanawake na wanaume.

 “Mkutano huo uliofanyika China mwaka 1995 ulichochea ukombozi wa wanawake angalau kwa sasa wameshika nafasi katika sekta nyingi za uongozi japo hakuna usawa ukilinganisha na wanaume,” anasema.

 Mkazi mwingine Mariamu Mungayi, anasema katika wilaya hiyo wananchi wanauelewa mdogo kuhusiana na masuala ya ukatili wa kijinsia na mifumo dume.

 Akizungumza na Nipashe  Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Lihundi, anasema wataendelea kutekeleza malengo ya Beijing kwa kushirikiana na mashirika yanayotetea haki za wanawake na usawa wa jinsia nchini.

 Anasema pia wataendeleza vuguvugu la kuwashawishi wanawake kuwania nafasi za uongozi ili wajitambue na waondokane na manyanyaso.

 Anabainisha kuwa lengo la kupeleka tamasha hilo Kondoa ni kutokana na takwimu kuonyesha wilaya hiyo bado ina tatizo la ukatili unaoendelea siku kwa siku.

 “Tunafahamu kwamba changamoto ya mimba za utotoni ni kubwa wilayani  Kondoa, wengi hawafahamu nini maana ya dira ya taifa ya maendeleo, lakini ni jambo linalohitaji juhudi kubwa kuanzia jamii na serikali.”

Anasema Mkuu wa Wilaya, Fatma Nyangasa, anasema ni changamoto na kwamba anafanya tathmini ya kina ili kuandaa mikakati ya kuukabili.

 “Ni matatizo ambayo kwa kiasi kikubwa yamejikita katika mila na desturi na yanahitaji nguvu za pamoja kufikia dira ya maendeleo ya mwaka 2050 mimba za utotoni iwe historia,” anasema Lilian.

 Kinachosemwa na Lilian kinaungwa mkono na mshauri mwelekezi katika masuala ya jinsia, sanaa na maendeleo, Agness Lukanga.

Akiwa na la ziada kwamba katika miaka 30 iliyopita tangu mkutano mkuu wa Beijing, upo uelewa mkubwa kuhusu masuala ya kijinsia. Ingawa matukio ya ukatili wa kijinsia yameongezeka, kasi ya kuripoti matukio hayo pia imeongezeka.

Agness anasema  kutokana na uelewa uliopo na sauti zinazopazwa, hatua mbalimbali zimechukuliwa na hata serikali imetengeneza mkakati wa kwanza wa kupinga na kupambana na ukatili.

Anakumbusha kuwa licha ya kuwapo kwa mwamko mkubwa wa kupaza sauti, bado kuna changamoto ambazo serikali inatakiwa kuzifanyia kazi.

Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Fatma Nyangasa, anawataka wananchi kuitumia vema elimu waliyoipata kupitia tamasha hilo, lenye ujumbe 'dira jumuishi ya 2050, miaka 30 Beijing tujipange'.