UTAFITI unaofanyika hivi karibuni umebaini kuwa kwa kila saa unayoketi iwe kuangalia runinga au kupiga gumzo kijiweni unapunguza uhai wako kwa dakika 22.
Sasa kazi kwako angalia unatumia saa ngapi kupiga umbea, kushinda kijiweni kwenye biashara za wenzako, au kuangalia runinga ukiwa umekaa na ufanya mahesabu dakika ulizopoteza kwenye miaka ya uhai wako.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukizwa Tanzania (TANCDA), licha ya kwamba utafiti huo haukufanyika Tanzania, wanasisitiza kuwa kuketi kwa zaidi ya saa moja mfululizo kuna athiri nyingi.
Mosi, kunaathiri uwezo wa mwili kuchakata sukari, huleta shinikizo la damu na mwili kutumia mafuta hivyo kuongeza uwezekano wa kuugua moyo, figo, kisukari na saratani.
Shirikisho linasema vile vile kuketi huko huongeza uwezekano wa mwili kushindwa kunyooka ipasavyo na kusababisha maumivu ya mgongo na hata kukunjika uzeeni.
Taarifa hizo zipo kwenye machapisho yao kuhusu magonjwa yasiyoambukiza pamoja na elimu ya utaalamu waliyotoa kwa wafanyakazi wa IPP Media, walipowatembelea kwa ushauri na vipimo vya maradhi ya kisukari.
Aidha, wataalamu wanasema kuketi muda mrefu kunaathiri afya ya akili na kushauri kuwa ni lazima kutembea, kujinyoosha kwa dakika mbili kila baada ya kuketi kwa saa moja.
Lakini pia wanashauri kuacha mtindo wa ubwete na kuushughulisha mwili, iwe kusimama, kutembea, kufanyakazi badala ya kujipumzisha kwenye viti.
Kwa mfano, umeanza kazi saa 3:00 asubuhi ikifika saa 4: 00 kama ulikuwa umekaa kwenye kiti ukihudumia wagonjwa, kufundisha darasani au kuchapa kazi kwenye kompyuta simama na tembea kuifanyisha misuli kazi.
Tembea umfuate mwenzako kueleza haja yako, achana kupiga simu au kutuma SMS, ukipigiwa simu au kupiga ongea ukiwa umesimama siyo kukaa muda wote.
“Pia punguza muda wa kuketi mfululizo kuangalia runinga, au kompyuta, kusogoa, badala yake ongeza muda wa kufanya mazoezi hasa kusimama wima badala ya kuketi.”
NDIKO KUJIMALIZA
TANCDA inakumbusha kuwa mwanadamu anapozaliwa misuli yake haijui kazi, kwani kwa miezi tisa ililala tumboni kwa mama bila shughuli.
Baada ya miezi sita tangu kuzaliwa, mtoto anaanza kukaa na zaidi ya mwaka mzima anahitajika kujifunza kutembea na kukimbia.
“Tunahitaji uzoefu kuendelea kutumia misuli yetu karibu kila siku ili kudumisha uzoefu huu. Bila shughuli misuli inasahau jinsi ya kutumia sukari na kutojishughulisha, ikumbukwe misuli isiposhughulishwa inasahau kutumia sukari na kutoshughulisha misuli ni moja ya visababishi vya kisukari, saratani, magonjwa ya moyo, na mishipa ya fahamu.”
Shirika la Afya Duniani (WHO), linakadiria kuwa kutokuushughulisha mwili kunachangia asilimia sita ya vifo vyote duniani, asilimia 17 ya magonjwa ya moyo, na kisukari asilimia 12 ya kuanguka kwa wazee na asilimia 10 ya saratani ya matiti na utumbo mpana.
Wataalamu wa magonjwa yasiyoambukiza wanaonya kuwa bila kuushughulisha mwili hauwezi kufanyakazi kakamilifu na ushauri wao ni kufanya mazoezi kama kutembea, kuendesha baiskeli, kushiriki michezo na burudani.
Kufanya mazoezi ni lazima ili misuli iwe imara angalau nusu saa kila siku. Zipo njia tano za kufanya mazoezi kila siku kwa mfano, ukiwa kazini, shuleni au nyumbani, kusafiri, kushiriki michezo, kucheza muziki na kazi za kijamii.
Inasisitizwa kuwa tendo lolote linalohusisha misuli na kuongeza mapigo ya moyo au kasi ya kupumua au mwili kutoka jasho, liwe ni kazi, kusafiri, michezo au burudani.
Kadhalika zinahitajika shughuli za kulainisha viungo, kuimarisha misuli na kutuwezesha kufanyakazi bila kuchoka haraka. Tunahitaji tuweze kukimbia, kuruka juu, wepesi kukata kona na kukwepa vitu bila kuanguka na pia kujikunja kama mtu atahitajika kupita sehemu nyembamba au kuketi chini sakafuni.
KULALA NI MUHIMU
TANCDA inashauri kulala kwa muda mahususi kulingana na umri, mathalani watoto wa miaka sita hadi 13 wanapaswa kulala saa tisa mpaka 11, wakati vijana wa miaka 14 hadi 17 watumie saa nane hadi 10 kulala.
Inashauri pia kwamba wenye miaka 14 hadi 64 walale saa saba mpaka tisa kila siku wakati wazee kuanzia miaka 65 walale kwa saa saba hadi nane.
“Jizoeshe kulala saa ile ile kila siku. Mfano kama ni saa 4:00 usiku fanya hivyo siku zote. Amka muda ule nyakati za asubuhi kama ni saa 11:30 hata kama ni sikukuu au likizo ama mwisho wa juma.” Inasema TANCDA.
Wataalamu hao wanakumbusha kuwa kuzingatia muda wa kulala kunajenga vichocheo au homoni za kukabiliana na msongo wa mawazo (sonona) na kuimarisha afya ya mwili.
Aidha, kunaondoa uwezekano wa kupata maradhi ya kisukari, shinikizo la damu, unene kupindukia, figo na sonona.
Ufanisi na usalama kazini na umakini darasani unapungua iwapo mtu hatalala vya kutosha.
ANGALIZO
TANCDA inawashauri Watanzania kuacha kutumia vitanda kwa shughuli zisizohusiana na kulala na eneo hilo liwe ni sehemu ya kupumzisha mwili.
“Usikitumie kitanda kuangalia runinga, kufanyakazi kwenye kompyuta, kuangalia simu, kuandika, kusoma magazeti na vitabu. Ni vyema ukaizoesha akili yako kuwa kitanda ni sehemu ya usingizi.” Inasema TANCDA.
Iwapo usingizi hauji, ondoka na kufanya kazi kitu kitakachofanya upumzike badala ya kuwaza changamoto zako, mfano kusoma vitabu vya hadithi, maandiko matakatifu lakini pia kufanya mazoezi mepesi.
Wanashauri urudi kitandani mara moja unapoona usingizi unaanza kuja.
KUVUTIA USINGIZI
TANCDA inashauri ili kuwa na mazingira ya kulala kwa furaha na utulivu punguza mwanga chumbani, ondoa kompyuta na runinga, pia chumba kiwe na hewa ya kutosha, kuwe na ubaridi na kuepuka kuangalia saa mara kwa mara kwani vinaondoa utulivu na kusababisha ushindwe kulala.
Wataalamu hawa wanashauri kuepuka kutumia muda mwingi kulala mchana au kusinzia kwenye kiti, daladala na kwingineko. Hii hupunguza muda wa kulala nyakati za usiku.
KUMBUKA MAZOEZI
Kufanyakazi au kuushughulisha mwili ni chanzo cha kubaki imara na kuonekana kijana kwa muda mrefu zaidi.
Kadhalika ni njia ya kudhibiti unene, kisukari na mafuta yaliyozidi mwilini na kuepusha shinikizo kubwa la damu, kisukari, magonjwa ya moyo na saratani.
Aidha ni muhimu kufanikisha kujanga misuli ambayo husaidia kutumia nishati ya ziada na hivyo kuepuka unene kupindukia.
Kuushughulisha mwili kunajenga mifupa imara na unyumbufu wa viungo badala ya kuwa vigumu na hata kukakamaa. Ni njia ya kupunguza msongo wa mawazo na uchovu.
Kadhalika huleta usingizi mnono, kuongeza kinga ya mwili na kuimarisha hisia huku ukiongeza ufanisi wa akili.
Aidha, ni dawa ya kuchelewa kwa mwamko au mlipuko wa dalili za magonjwa ya akili kama sonona na wasiwasi, pamoja na kupunguza dalili nyinginezo za maradhi ya akili.
Kiwango cha mazoezi kinacholeta faida ni shughuli isiyopungua dakika 30 kwa siku angalau siku tano kwa wiki. Hizo dakika 30 zinaweza kuchukuliwa kwa vipindi tofauti.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED